Language

Monday 14 January 2013

HABARI: VIFO VYA MAMA NA MTOTO SAS BASI


MAKAMU wa Rais Dkt. Mohamed Gharib Bilal, leo anafungua mkutano wa kimataifa wa Afya ya Mama ambao utahusisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 68 wakiwemo wanasiasa.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana, Mkurugenzi wa Asasi ya Management and Development for Health (MDH), Dkt. Chalamila Guerino, alisema mkutano huo utakuwa na manufaa kwa afya ya wanawake wajawazito ambao kila siku wanapoteza maisha wakati wa kujifungua.Alisema mkutano huo utakuwa wa siku tatu, utajadili changamoto mbalimbali wanazopata wajawazito kwenye uzazi na utafungwa Januari 17 mwaka huu na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete.“Mkutanio huu utakuwa na washiriki wasiopungua 700, wakiwemo wanasiasa ambao watapewa mbinu mbalimbali zitakazowasaidia kujua masuala ya afya ya mama ili kupunguza vifo vinavyotokea.“Wanasiasa watapewa mbinu na elimu ya kuzungumza na wananchi ili jamii iweze kuepukana na vifo vinavyochangia umaskini nchini,” alisema Dkt. Guerino.Akizungumzia vifo vya wajawazito hasa wakati wa kujifungua, alisema Tanzania bado inakabiliwa na changamoto hasa maeneo ya mijini ambayo vifo ni vingi.“Takwimu za kidunia nazo zinaonesha kuwa, asilimia kubwa ya wanawake wanapoteza maisha hasa wakati wa kujifungua, nchini Tanzania wanawake 454, kati ya 100,000 hufariki dunia wakati wa uzazi huku.“Kwa nchi zinaendelea duniani, wanawake 300,000 hufariki dunia hivyo tunapaswa kupambana na hali hii haraka kwa kuhusisha makundi mbalimbali pamoja na wanasiasa,” alisema.Alisema kwa upande wa mijini nchini, changamoto bado ni nyingi ambapo ili vifo hivyo viweze kuwa historia, lazima tuwe na umoja ambao ni thabiti ili kuokoa maisha ya wanawake.Aliongeza kuwa, mkutano huo pia utajadili upatikanaji wa vitendea kazi ili kuboresha huduma ya afya kwa wajawazito na upimaji ubora ambapo kupitia mada hizo, Tanzania itaweza kuepusha vifo vingi vya wanawake wajawazito.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...