Language

Sunday 14 April 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: SHILINGI BILIONI 620 ZA DENI LA TAIFA HAZINA MAELEZO



 


Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
ametoa taarifa yake ya mwaka 2011/2012 na kuonyesha kuwa kuna skandali kubwa
sana katika akaunti ya Deni la Taifa. Nanukuu

‘Uhakiki wa mchanganuo wa madeni ya Taifa kama ulivyokuwa tarehe 30
Juni, 2012 ulibaini kuwepo kwa marekebisho ya deni ya shilingi
619,803,554,183.91 ambayo uongozi haukuweza kutoa maelezo ya kuridhisha.’
(Taarifa ya CAG, Ripoti ya Serikali Kuu 2011/2012 uk 158). Mwisho wa Kunukuu.

Katika Taarifa yake hiyo CAG anaendelea kuonyesha
kuwa Deni la Taifa linazidi kukua na mwaka unaoishia mwezi Juni 2012 deni
lilikuwa kwa asilimia 17 kutoka mwaka unaoishia mwezi Juni 2011.
Kukosekana kwa maelezo ya kuridhisha kuhusu zaidi

ya nusu trilioni za Deni la Taifa ni jambo linalopaswa kutiliwa mashaka
makubwa, kuchunguzwa na kupata majawabu stahiki. Tafiti mbalimbali duniani
zinaonyesha kuwa kuna mahusiano makubwa sana kati ya Deni la Taifa la
utoroshaji wa fedha kwenda kwenye mabenki ya ‘offshore’. Katika kitabu cha
‘Africa’s Odious Debts: How Foreign Loans and Capital flight bled a continent’
kilichoandikwa mabwana Leonce Ndikumana na James Boyce imeonekana kwamba Deni
la Taifa huchochea utoroshwaji wa Fedha kwenda kuficha nje ya Tanzania.

Mabilioni haya kwenye akaunti ya Deni la Taifa
yanashtusha sana. Kambi ya Upinzani Bungeni kwa miaka miwili mfululizo imekuwa
ikitaka ukaguzi maalumu kwenye akaunti za Deni la Taifa lakini Serikali
imeshindwa kufanya hivyo. Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya PAC pia nimemtaka CAG
afanye ukaguzi huu maalumu.
Kambi ya upinzani Bungeni ilisema hivi katika
Bajeti yake kivuli 2012/13:

DENI LA TAIFA

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitika kwa serikali kuendelea kutengeneza
madeni kwa Taifa kwa kuendelea kukopa zaidi kwa matumizi ya kawaida ya
serikali. Wakati Serikali inasisitiza kwamba Deni letu linastahmilika, Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Serikali anaonyesha mashaka makubwa sana kutokana na kasi ya
kukua kwa Deni la Taifa. Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali inaonyesha  kuwa Deni la Taifa
linazidi kuongezeka kwa asilimia 38% kutoka shilingi trillion 10.5 mwaka
2009/2010 hadi shilingi trillion 14.4 mwaka 2010/2011. Kwa mujibu wa Waziri wa
Fedha Deni la Taifa limefikia shilingi trillion 20.3 mpaka ilipofika mwezi
Machi mwaka 2012. Ukisoma taarifa ya Mwezi wa Mei 2012 ya Benki Kuu ya
Tanzania, Deni la Taifa sasa limefikia shilingi trillion 22.




Mheshimiwa Spika, Suala hapa sio ustahmilivu wa
Deni kama inavyodai Serikali bali ni kwamba tunakopa kufanyia nini? Bajeti ya
Mwaka 2012/13 inayopendekezwa inaonyesha kwamba Serikali itakusanya shilingi
trilioni 8.7 kama makusanyo ya ndani na itatumia shilingi trilioni 10.6 kama
matumizi ya kawaida. Ni dhahiri kwamba sehemu ya mikopo ambayo serikali
inachukua sasa itakwenda kwenye matumizi ya kawaida. Hatutaki mikopo kwa ajili
ya matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari nk. Tuchukue mikopo kuwekeza
kwenye miradi itakayokuza uchumi na kuzalisha kodi zaidi. Bajeti inaonyesha kwamba
Serikali itakopa shilingi takribani trillion 5 mwaka 2012/13.  Serikali ikubalikutekeleza mapendekezoya
Kambi ya Upinzani ya kuimarisha ukusanyaji
wa kodi na kupanua wigo wa kodi katika maeneo muhimu kama sekta ya
madini na mawasiliano, kuzuia misamaha ya kodi, kutokomeza ukwepaji kodi, na
kuepuka matumizi mabaya ili kuepuka madeni yasiyo ya lazima.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapenda
kusisitiza kwamba Bunge lifanye ukaguzi maalumu kuhusu akaunti ya Deni la Taifa
ili kuweza kubaini ukweli kuhusu ustahmilivu wa Deni na mikopo ambayo Serikali
inachukua kama inakwenda kwenye Maendeleo na miradi ipi na kama miradi hiyo ina
tija. Vilevile tumependekeza kwamba Mikopo yote ambayo Serikali inachukua iwe
inapata idhini ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi au Bunge litunge sharia
ili kiwango cha juu cha kukopa ambacho Serikali haipaswi kuvuka. Kuiacha
Serikali inaendelea kukopa bila mpango ni kuliweka Taifa rehani na kupeleka
mzigo wa kulipa madeni haya kwa kizazi kijacho. Hatuwezi kukubali Wazee wetu waishi maisha yao, waishi maisha yetu na
pia wakope maisha ya watoto wetu. Mwisho wa
kunukuu.

Kambi ya Upinzani inarejea kutaka
ukaguzi maalumu kuhusu akaunti za Deni la Taifa na maelezo ya kina ya Serikali
kuhusu shilingi 620 bilioni ambazo hazina maelezo kwenye Deni la Taifa.
Hatuwezi kukaa kimya kuona Watanzania wanabebeshwa madeni ambayo kimsingi ni
madeni bandia yanayotajirisha watu wachache wenye uwezo na ujasiri mkubwa wa
kuiba, kupora nakufisidi hazina ya Taifa letu.

Kabwe
Zuberi Zitto,Mb
Waziri Kivuli Fedha na Uchumi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...