Language

Thursday 28 February 2013

HABARI MUHIMU: TABIBU ALIYEMTOA MIMBA BAAMEDI KUPANDISHWA KIZIMBANI

POLISI Bunda wamesema watamfikisha mahakamani wakati wowote Ofisa tabibu mmoja wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, anayetuhumiwa kumtoa mimba mhudumu mmoja wa baa ambaye kwa sasa hali yake ni mbaya.

Ofisa tabibu huyo Michael Musimu, ambaye amekuwa akifanya kazi katika kituo cha afya Manyamanya, kilichoko Bunda, anashikiliwa na polisi akituhumiwa kumtoa mimba  mhudumu mmoja wa baa ijulikanayo kwa jina la Savana, iliyoko mjini hapa.
Polisi wamemtaja mhudumu huyo kuwa ni Salome Saimon Bugunda, ambaye sasa hali yake ni mbaya na amepelekwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando Mwanza kwa matibabu zaidi.
Imedaiwa kuwa tukio hilo lilitokea juzi na kwamba baada ya Musimu kumtoa mimba mhudumu huyo, hali yake ilibadilika na kumpeleka katika kituo cha afya Manyamanya, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya zaidi na ndipo akakimbizwa katika hospitali ya DDH Bunda ambako pia alipewa rufaa ya kwenda Bugando.
Aidha, imeelezwa kuwa mhudumu huyo ameumizwa vibaya kwani sehemu ya utumbo wake umetoka nje.
Kukamatwa kwa ofisa tabibu huyo kumetokana na mwanamke huyo kumtaja bayana kwa kuwaambia ndugu zake ambao walitoa taarifa polisi. Licha ya polisi kuthibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kumshikilia mtuhumiwa huyo, lakini Kamanda wa Polisi Mara, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Absalum Mwakyoma amesema bado hajapatiwa taarifa kamili juu ya tukio hilo na kuahidi kulifuatilia.

HABARI MUHIMU: MAGARI YA ZIMAMOTO YAMETAJWA KUVUSHA MALI ZA WIZI UWANJA WA NDEGE WA JK NYERERE DAR

IMEBAINIKA kuwapo kwa wizi wa kutisha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, huku magari ya Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji yakitajwa kwamba yamekuwa yakivusha vifaa vya wizi kutoka ndani ya uwanja huo.

Wizi huo ambao umewasababishia hasara kubwa baadhi ya wasafiri wakiwamo wafanyabiashara, abiria wa kawaida na watalii wanaoingia nchini, unadaiwa kufanywa na baadhi ya wafanyakazi wa Wakala wa Mizigo wa Kampuni ya Swissport.
Wafanyakazi hao wamekuwa wakiiba vifaa na bidhaa kwa kuchana mabegi ya abiria kisha kuviweka kwenye makoti yao ya kazi lakini kwa mizigo mikubwa, wamekuwa wakiificha kwenye magari ya zimamoto ambayo huingia na kutoka ndani ya uwanja wa ndege bila kufanyiwa ukaguzi.

HABARI MUHIMU: ZAIDI YA DOLA 377,000 ZIMETUMIKA KUNUNUA IPAD BUNGENI


BUNGE nchini Uganda limetumia zaidi ya dola 377,000 kununa kompyuta aina ya iPad kwa ajili ya wabunge wote .

Maofisa wa bunge hilo walisema kuwa mbali na kuwaweka wabunge hao karibu na ulimwengu wa teknolojia, wanatarajia kuwasaidia kupunguza gharama za fedha zinazotokana na matumizi ya uchapishaji wa nyaraka mbalimbali.
Kamishna wa bunge hilo Elijah Okupa alisema kuwa kompyuta hizo ni bora na zinafaa kwa matumizi hivyo ni vyema zikatumiwa vizuri.
Alisema iPad hizo zitakuwa ni mali ya wabunge lakini kama mtu atatumia kwa muda wa miaka mitano asitegemee itakuwa na ubora uleule wa kumwezesha mwingine atumie kwa miaka hiyo alisema Okupa
Kwa mujibu wa takwimu kutoka katika bunge hilo zilionyesha Serikali imekuwa ikitumia zaidi ya dola 12 katika miaka miwili sasa kwa ajili ya mahitaji ya kama kompyuta, uchapishaji wa nyaraka, mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha mawasiliano kuwa bora katika bunge.
Kwa mujibu wa mbunge kutoka mashariki, Medard Segona alisema kuwa kutokana na uwepo wa ipad hizo wanategemea kupunguza matumizi ya fedha zilizokuwa zikipotea hapo awali.
‘’Vifaa hivyo vitapunguza sana matumizi ya fedha kwa kuwa hapo awali wizara ya fedha ilikuwa ikichapisha zaidi ya nyaraka 400 kwa kila mbunge na maofisa wengine waliopo ndani ya bunge hilo’’alisema
Aliongeza kuwa komputa hizo ni muhimu kwa utendaji kazi hasa katika kipindi hicho cha kuendeleza matumizi ya teknolojia.
Hata hivyo taarifa zilisema kuwa wabunge hao bado hawana uelewa mzuri juu ya matumizi hayo licha ya kuwa kampuni imeahidi kutoa mkataba wa mafunzo ambayo pia yatasaidia kupunguza gharama za matumizi.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...