Wanachama wote wa Baraza la usalama la Umoja wa
Mataifa wameunga mkono harakati za jeshi la Ufaransa dhidi ya wapiganaji
wa kiisilamu nchini Mali.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
alisema kuwa anatumai hatua ya jeshi hilo itaweza kurejesha utulivu na
uthabiti nchini humo.
Maelfu ya wanajeshi wa Afrika
wanatarajiwa kujiunga na harakati za kijeshi dhidi ya Wapiganaji nchini
Mali kusaidiana na wanajeshi wa Ufaransa.
Ufaransa iliingilia mzozo huo siku ya Ijumaa baada ya wapiganaji kuanza kusonga mbele Kusini mwa nchi.
Maafisa wa utawala nchini Ufaransa, walisema
kuwa wanahofia waasi huenda wakaukaribia mji mkuu Bamako na kusababisha
tisho kubwa la usalama katika eneo hilo zima.
Siku ya Jumatatu , baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, lilifanya mkutano mjini New York kufuatia ombi la Ufaransa.
Baada ya mkutano, balozi wa Ufaransa katika
Umoja wa Mataifa,Gerard Araud alisema kuwa nchi yake inaungwa mkono na
wanachama wote wa baraza la usalama.
Lakini aliongeza kuwa Ufaransa pia ilitaka wanajeshi wa nchi za Afrika Magharibi kupelekwa Mali mara moja.
Hatua ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa
kuunga mkono jeshi la Ufaransa ni ishara ya wasiwasi mkubwa uliopo
kuhusu uwezo wa makundi ya kiisilamu yaliyojihami nchini Mali.
Wanadiplomasia wanaonekana kuwa na wasiwasi
kuhusu kuwasili kwa wanajeshi nchini Mali kusaidia na harakati za jeshi
la Mali dhidi ya waasi.