Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeingilia kati wizi wa fedha kwa kutumia
mashine za kutolea fedha (ATM), ambao umeibua hofu kubwa katika sekta ya benki
nchini.
Kutokana na wizi huo kukithiri katika baadhi ya benki, wafanyabiashara na wananchi wameanza kujipanga kuondoa fedha zao katika akaunti.
Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu alizungumza kwa njia ya simu mwishoni mwa
wiki kwamba wameziagiza benki kuweka kifaa cha umeme (electronic chip) kwenye
kadi zao za ATM ambazo si rahisi kughushi.
“Wizi kama huo unatokea wakati mtu anaweka namba za siri kwenye ATM kwani kuna
watu huweka kamera ambazo husoma na namba hizo kufanikiwa kuzipata kisha
kufanya wizi ,” alisema Profesa Ndullu.
Alisema kuwa kutokana na wizi kukithiri wamezitaka benki zote kuweka mifuniko
katika eneo la namba za siri ili wezi wanaoweka kamera ili kuzinasa wakati mtu
anatoa fedha washindwe kufanya hivyo.