Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kwa gharama yoyote
kipo tayari kumtetea Mkurugenzi wake wa Ulinzi na Usalama, Wilfred Lwakatare
dhidi ya kesi ya ugaidi inayomkabili.
Lwakatare na mwenzake, Joseph Rwezaura, wanakabiliwa na kesi ya ugaidi katika Mahakama ya Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka manne ya kula njama na kufanya mipango ya kumteka, kisha kumdhuru kwa sumu, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.
Majalada hayo namba 37 na namba 6 yote ya mwaka 2013, yalishawasilishwa
Mahakama Kuu, kwa awamu mbili. Jalada la kwanza, namba 37 liliwasilishwa
Mahakama Kuu, Jumatatu na jalada la pili namba 6 liliwasilishwa Jumanne wiki
hii iliyopita.
Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu
alisema kuna wanaohoji nguvu ya kisheria wanayoitumia kuweka jopo la mawakili
watano kumtetea Lwakatare, akisisitiza kuwa wapo tayari kuhakikisha sheria
inatumika ipasavyo kubainisha ukweli wa tuhuma hizo.
Lissu aliyasema hayo jana alipokuwa akieleza msimamo wa baadhi ya mambo
yaliyojadiliwa na Kamati Kuu kwenye kikao chake kilichofanyika Dar es Salaam.