Mgambo wa jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa), anashikiliwa polisi
kwa tuhuma za kuhusika katika njama za mauaji ya mwendesha Bajaji Yohana
Syprian aliyeuawa jana Kawe jijini Dar es Salaam.
Mgambo huyo ambaye alitambuliwa kuwa ni mlinzi wa maduka ya Bakhresa,
inasemekana kutumiwa kama njia ya kumtafuta dereva wa bajaji aliyetuhumiwa
kuiba simu hiyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyera
alisema mgambo huyo atahojiwa na kutumika ili kuwapata wahalifu hao.
“Inasemekana marehemu alikuwa ni mpitanjia tu wakati vurugu zinaendelea
katika kijiwe hicho, wakaamua kumshambulia yeye mpaka mauti yalipomkuta na
baadaye wakamtupa kwenye Mto Mbezi,” alisema Kamanda Kenyera.
Kenyera alisema polisi wanafanya uchunguzi kuhakikisha wanajeshi hao
wanaodaiwa kuhusika wanakatwa na kufikishwa mahakamani.
‘‘Huyu mgambo atatusaidia kuwapata kwa urahisi,” alisema na kuongeza:
“Si hivyo tu, pia tunawashikilia vijana wengine 12 waliokuwa wanafanya vurugu
za kutaka kuchoma moto Kituo cha Polisi.”
Kamanda Kenyera alisema kushikiliwa kwa vijana hao kunatokana na
kitendo cha kukosa uvumilivu baada ya mgambo huyo kubainika na kosa hilo na
kwamba ndipo kundi la vijana wa Kawe waliamua kumfuata nyumbani kwake ili
wamshambulie na kumuua.
“Polisi walikuwa wameshapata taarifa hizo na kufika haraka nyumbani
kwake, tulikuta wanataka kuchoma moto ile nyumba ila mwenye nyumba akawashauri
wamtoe, kilichosaidia ni kufika mapema pale vinginevyo wangemuua.
Alisema baada ya polisi kumchukua mgambo huyo hali ilibadilika na
wananchi hawakukubaliana na uamuzi huo jambo lililosababisha kuandamana mpaka
Kituo cha Polisi cha Kawe na kutaka kukichoma moto.
Polisi waliamua kutumia nguvu ya ziada baada ya kuongeza idadi ya
Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) ili kutuliza vurugu hizo.
Kuanzia saa 10:00 jioni mpaka saa 3:00 usiku hali ya fujo ilikuwa
imetanda katika mitaa yote huku barabara iendayo Kituo cha Mwenge ikiwa
imefungwa kwa muda.
Zaidi ya magari sita ya askari hao yalikuwa yakirandaranda na kulipua
mabomu ya machozi huku gari la maji ya kuwasha likiendelea kusafisha mitaa
mpaka pale hali ilivyotulia.
No comments:
Post a Comment