Vikosi vya uokoaji vinasema, watu wapatao 30 wamefariki dunia na mamia
wengine wanahofiwa kukwama baada ya jingo la ghorofa nane kuporomoka katika mji
mkuu wa Bangladesh, Dhaka.
Juhudi za ziada zinaendelea kuwaokoa watu walionaswa kwenye kifusi.
Watu wapatao 200 wamejeruhiwa kufuatia ajali hiyo. Jeshi linasaidia shughuli za
uokoaji katika eneo la tukio nje kidogo ya jiji la Dhaka.
Matukio ya majengo kuporomoka nchini Bangladesh ni ya kawaida kutokana
na majengo mengi marefu kujengwa kinyume na sheria za ujenzi.
Jengo lililoporomoka lilikuwa na kiwanda cha nguo, benki na maduka
kadhaa. Liliporomoka asubuhi wakati watu wakielekea makazini.
Watu wengi wamekusanyika karibu na eneo la tukio wakiwatafuta ndugu na
marafiki. Mwandishi wa BBC mjini Dhaka anasema haijafahamika kilichosababisha
jengo hilo kuporomoka, lakini vyombo vya habari nchini humo vimearifu kwamba,
nyufa zilionekana kwenye jengo hilo siku ya Jumanne.