Bomu limelipuka nje ya ubalozi wa Ufaransa katika mji mkuu wa Libya,
Tripoli na kuwajeruhi walinzi wawili huku ikisababisha uharibifu mkubwa.
Mlipuko huo ulisababisha uharibifu katika sehemu moja ya ofisi hizo na
pia kuharibu nyumba jirani.
Mwandishi wa BBC mjini Tripoli, Rana Jawad anasema kuwa inaaminika kuwa
mlipuko huo ulisababishwa na gari lililokuwa na mabomu.
Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, aliitaka serikali ya Libya
kuchukua hatua za haraka kukabiliana na waliosababisha shambulio hilo.
Aliongeza kwamba shambulizi hilo lililenga nchi za kigeni zinazopambana
dhidi ya ugaidi.
Balozi za kigeni nchini Libya zimewahi kushambuliwa katika siku za
nyuma, lakini hili ndilo shambulizi la kwanza kubwa dhidi ya ubalozi wa kigeni
mjini Tripoli.
Shambulizi liliwahi kufanywa dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini
Benghazi mwezi Septemba mwaka jana na kusababisha kifo cha balozi Christopher
Stevens pamoja na maafisa wengine wamarekani .
Shambulio la leo lilifanyika muda mfupi baada ya saa kumi na moja asubuhi
katika mtaa wa kifarahari mjini Tripoli.
Wakaazi wa eneo hilo walighadhabishwa sana na shambulizi hilo na
kulalamikia ukosefu wa ulinzi mzuri wa sehemu hiyo.
Waziri wa mambo ya nje wa Libya, Mohammed Abdel Aziz alilaani vikali
shambulizi hilo, ingawa hawajaeleza ni nani wanayemshuku kulifanya.
No comments:
Post a Comment