Haya ni baadhi ya matukio muhimu yaliyotokea katika viwanja vya michezo katika mwaka wa 2012, ikiwa ni pamoja na kandanda, michezo ya Olimpiki jijini London, riadha na kadhalika
Tunaanza uchambuzi wetu katika viwanja vya kandanda ambapo, ushindi wa tatu mfululizo wa Uhispania, katika kinyang'anyiro kikuu na umaahiri wa kibinafsi wa ufungaji mabao wake Muargentina Lionel Messi ni matukio yatakayokumbukwa katika madaftari ya mwaka wa 2012. Lakini mwaka huo pia ulikumbwa na mikasa ya vifo vya Misri na Uholanzi na wasiwasi wa ongezeko la matukio ya kibaguzi katika kandanda barani Ulaya.
Ni mwaka ambao pia ulimwengu wa soka ulibadilika kutoka enzi za karne ya 19, na kuingia katika karne ya 21 wakati teknolojia ya kubainisha iwapo mpira umevuka mstari kwenye lango ilipoidhinishwa na shirikisho la soka ulimwenguni FIFA. Mbinu hii ilitumiwa rasmi kwa mara ya kwanza katika mashindano ya fainali za Klabu bingwa ulimwenguni nchini Japan. Katika dimba hilo, klabu ya Corinthians kutoka Brazil iliibuka kidedea kama klabu bora ulimwenguni, taji ambalo natumai kila mmoja wetu atakubali kwamba linapaswa kuwaendea Barcelona wa Uhispania.
Lakini mojawapo ya mishangao mikubwa iliyotokea katika mwaka huu, Barcelona walishindwa kutwaa kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya- UEFA Champions League, ambalo lilionekana kuwa lao, kabla ya kuduwazwa na Chelsea katika nusu fainali, wakati Messi alipodhihirisha kuwa kumbe yeye pia ni binaadamuu na wala siyo kiumbe kilichozaliwa nje ya dunia, aliposhindwa kufunga penalti. Hata hivyo Messi alimaliza mwaka kwa kufunga magoli 91, ikiwa ni rekodi mpya kabisa ulimwenguni, baada ya kuifuta ile iliyowekwa na mshambuliaji wa zamani wa Ujerumani Gerd Mueller iliyodumu miaka 40.
Chelsea ambao walimaliza Premier League ya England wakiwa katika nafasi ya sita mwezi Mei, walienda moja kwa moja na kunyakua taji la Champions league katika fainali mjini Munich. Baada ya kufutiliwa mbali kabisa na vyombo vya habari vya Ulaya kabla ya kucheza dhidi ya Barca, waliwaduwaza tena wakosoaji kwa kuwazaba Bayern Munich kwa mikwaju ya Penalti katika uwanja wao wa Allianz Arena na kuwa klabu ya kwanza ya London kunyanua kombe hilo la Ulaya katika historia yake ya miaka 57.
Kando na kushinda pia kombe la FA, miezi sita baadaye, Roberto Di Matteo akapigwa kalamu na mmliki bwenyenye Roman Abramovich kabla ya klabu hiyo kuwa bingwa mtetezi wa kwanza kuondolewa katika dimba la Champions league. Aidha kukawa na matukio ya John Terry kuhusika katika madai ya kumtlea mchezaji matamshi ya kibaguzi. Uhispania waliwazaba Italia magoli manne kwa sifuri katika fainali ya kombe la Mataifa ya Ulaya, UEFA EURO 2012, yaliyoandaliwa Ukraine na Poland. Real Madrid kisha wakawapiku Barca katika La Liga, lakini msimu huu Barca wamerejea tena kileleni mbele kabisa ya Real.
Lakini kuna muujiza uliotokea baada ya aliyekuwa mchezaji wa Bolton Fabrice Muamba, alipozirai uwanjani wakati wa mchuano wa Premier League dhidi ya Tottenham Hotsour uwanjani White Heart Lane. Madaktari walisema Muamba alikufa kwa dakika 78, na kuutaja kurejesha fahamu kwake kuwa muujiza mkubwa. Tukio hilo limemfanya Muamba kuwachana na mambo ya soka kutokana na ushauri wa madkatari. Aidha katika matukio mengine mwaka ya mwaka, Zambia waliibuka kidedea katika dimba la mataifa ya Afrika lililoandaliwa Gabon na Guinea ya Ikweta. Chipolopolo jinsi wanavyohamika, waliwalaza Cote d'Ivoire waliokuwa wamepigiwa upatu zaidi kulishinda kombe hilo, magoli 8 – 7 kupitia mikwaju ya penalti baada ya mchuano kukamilika sare ya bila kufungana katika muda wa ziada.
Dortmund ilikuwa timu ya kwanza kando na Bayern, kuhifadhi taji la Bundesliga tangu ilipofanya hivyo miaka 16 iliyopita, na kumaliza desturi ya Bayern ya kushinda taji la ligi karibu kila msimu wa pili tangu mwaka wa 1996. Dortmund ilinyakua taji lake la nane la ligi ya Ujerumani wakati ilipoendeleza rekodi ya Bundesliga ya kutoshindwa katika mechi 26 mfululizo. Na walimaliza msimu kwa kuwa mabingwa mara mbili, yaani Bundesliga, na DFB Pokal. Hata hivyo kando na kufanya vyema katika jukwaa la Ulaya, Champions League, Dortmund wanaonekana kuwa wamesalimisha taji kwa Bayern ambao wamemaliza nusu ya kwanza ya msimu wakipepea kileleni na hawaonekani tena kukubali kuangusha pointi, ligi itakapoanza baada ya mapumziko ya msimu wa baridi
Michezo ya Olimpiki London 2012
Uingereza ilitumia takribani kiasi cha pauni bilioni tisa kuandaa viwanja vya kuvutia kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 2012, ambako mashabiki waliburudishwa kote jijini London kutokana na maandalizi ya michezo hiyo. Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron alisema baada ya mashindano hayo kwamba, wameuonyesha ulimwengu kile walicho nacho, na kujikumbusha wao kile wanachoweza kufanya.
Katika kandanda upande wa wanawake, Marekani iliwapiku Japan katika fainali magoli mawili kwa moja, na kunyakua dhahabu ya tatu mfululizo katika olimpiki. Na kwa upande wa wanaume, washindi mara tano wa Olimpiki Brazil, waliwachwa kinywa wazi baada ya kuzabwa na Mexico. Andy Murray hatimaye aliweza kupata ushindi wa Wimbledon katika fainali ya kuvutia dhidi ya Roger Ferderer. Katika mpira wa kikapu miamba wa Marekani katika NBA waliwanyamzisha Uhispania katika fainali na kuhifadhi taji lao la olimpiki
Sebastian Vettel atawala Formula One
Lance Armstrong apokonywa mataji
Bila shaka tukio jingine kuu lililotokea katika mwaka wa 2012, na ambalo litakumbukwa na wengi ni sakata iliyomkumba mwendeshaji basikeli maarufu Lance Armstong. Sakata hiyo iliwacha pengon kubwa katika madaftari ya kumbukumbu katika mchezo wa uendeshaji baisikeli, na kuchafua kabisa hadhi ya mchezo huo. Armstrong alipigwa marufuku ya maisha na kupokonywa mataji yake yote saba ya mashindano ya Tour de France baada ya shirika la Marekani la kupambana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli – USADA kufichua kile ilichosema kuwa ni mbinu yenye ujuzi wa hali ya juu ya matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku kuwahi kupatikana. Hata hivyo Armstrong alitangaza kuwa hataweza tena kupinga madai hayo ya matumizi ya dawa haramu, baada ya jaji kukataa kuisimamisha shughuli hiyo ya kumchunguza. Mwendeshaji baiskeli huyo Mmarekani alishinda mataji hayo saba ya Tour de France kutoka mwaka wa 1999-2005. Armstrong alidaiwa kuchukua usukani kabisa ambapo vyumba vya hoteli vilibadilishwa kuwa hifadhi za damu, madaktari wakalipwa nao waendeshaji baiskeli wakaonywa dhidi ya kufanya vipimo vya mapema kabla ya mashindano. Lance Armstrong ambaye ni mwathiriwa wa saratani, aliiuduwaza ulimwengu wa undeshaji baiskeli kutokana na umahiri wake.
Klitschko mabingwa wa ndondi
Tukisalia na mambo ya ndondi, ni kwamba suali kubwa linalosalia kuulizwa na mashabiki katika mwaka wa 2013, ni Nani anayeweza kuwasimamisha ndugu wawili Klitschko katika kitengo cha uzani wa heavyweight? Kwa sasa hakuonekani mpinzani anayeweza kufanya hivyo.
Baada ya kushikilia mataji ya WBA, IBF, IBO na WBO kwa miezoi 18 iliyopita, Wladmir Klitschko alipata ushindi wake wa 69 katika taaluma yake mnamo mwezi Novemba wakati alipopata ushindi kupitia wingi wa pointi dhidi ya Mariusz Wach wa Poland. Kama kawaida kulikuwa na uvumi kuhusu pigani baina ya pengine Witali, bingwa wa WBC au Wladmir dhidi ya David Haye wa Uingeerza, ambaye alirudi tena ulingoni baada ya kustaafu na kumrambisha sakafuni kwa njia ya knock put David Chisora mwezi Julai.