Kituo cha Afya ya Akili cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kilichopo
Chamazi Mbagala kina uwezo wa kuhudumia wagonjwa saba tu imefahamika.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha wagojwa wengi wenye tatizo hilo
kushindwa kupata huduma au kupata katika hali isiyo na ubora.
Akijibu swali bungeni jana, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Agrey Mwanri, alisema awali kituo
hicho kilikuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 32.
Mwanari alisema kutokana na kituo hicho kuwa na uwezo wa kuhudumia
wagonjwa wachache, Hospitali ya Muhimbili haipeleki wagonjwa katika kituo hicho
kama ilivyokuwa siku za nyuma.
Mwanri alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi
(CCM), aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuendeleza kituo hicho ambacho ni
muhimu kwa wagonjwa wa akili.