Mshindi wa mbio za mwaka 2012 za Boston Marathon, Wesley Korir,
aliyemaliza wa tano mwaka huu, ameambia BBC kuhusu hofu yake pindi aliposikia
milipuko miwili iliyotokea Boston Marekani.
Milipuko hiyo ilitokea karibu na msitari wa mwisho wa kumalizia mbio
hizo na kuwajeruhi takriban watu 140 takriban saa mbili baada ya mshindi
kumaliza mbio hizo.
''Ikiwa shambulio hilo lingetokea saa mbili kabla ya mbio kumalizika
labda ningekuwa miongoni mwa waliojeruhiwa,'' alisema bwana Korir.
Alikuwa akisherehekea ushindi wa mkenya Rita Jeptoo katika mbio za
wanawake.
"furaha yetu ni kuwa tulikuwa tayari tumeondoka katika eneo
hilo,'' Korir aliambia BBC.
Bi Jeptoo anatoka katika eneo bunge la Cherangany, ambalo bwana Korir
ni mbunge wake baada ya kushinda katika uchaguzi uliofanyika mwezi jana.
Licha ya milipuko hiyo pamoja na jukumu lake la kisiasa, Korir amesema
kuwa ataendelea kushindana katika mbio za marathon hata ikiwa Boston itaandaa
mbio zengine mwaka ujao.
Korir alisema kuwa aliogopa sana aliposikia kuhusu habari ya milipuko.
Alisema kuwa punde tu baada ya kusikia habari hiyo aliwapigia simu wakwe
zake kuwajulia hali kwani walikuwa wamemtembelea pamoja na kocha wake.
Balozi wa Kenya nchini Marekani amesema kuwa hana taarifa zozote kuhusu
wakenya waliojeruhiwa kwenye mashambulizi hayo.
Raia wawili wa Afrika Kusini walitibiwa baada ya kupata majeraha
Lelisa Desisa, wa Ethiopia alishinda mbio za wanaume mbele ya mshindani
wake Micah Kogo.
Mbio hizo mwaka huu zilikuwa na wanariadha 23,000 na zilitazamwa na
mamia ya mashabiki.
No comments:
Post a Comment