Kituo cha Afya ya Akili cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kilichopo
Chamazi Mbagala kina uwezo wa kuhudumia wagonjwa saba tu imefahamika.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha wagojwa wengi wenye tatizo hilo
kushindwa kupata huduma au kupata katika hali isiyo na ubora.
Akijibu swali bungeni jana, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Agrey Mwanri, alisema awali kituo
hicho kilikuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 32.
Mwanari alisema kutokana na kituo hicho kuwa na uwezo wa kuhudumia
wagonjwa wachache, Hospitali ya Muhimbili haipeleki wagonjwa katika kituo hicho
kama ilivyokuwa siku za nyuma.
Mwanri alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi
(CCM), aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuendeleza kituo hicho ambacho ni
muhimu kwa wagonjwa wa akili.
Naibu Waziri alisema, Hospitali ya Muhimbili inaendela na juhudi za
kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho, ili kutoa huduma kwa
wagonjwa wengi zaidi.
“Mpango wa baadaye kwa ajili ya kituo hicho ni pamoja na kukiendeleza
ili kiweze kutoa huduma kwa wagonjwa walioathirika na dawa za kulevya, alisema
Mwanri.
Alivitaja vituo vingine vinavyotoa huduma ya aina hiyo ni Kituo cha
Hombolo Dodoma ambacho ni sehemu ya Hospitali ya Milembe na Lutindi kilichopo
Korogwe ambacho kinamilikiwa na Shirika la dini.
Alisema Muhimbili imeanza utaratibu wa kupata mshauri mwelekezi ili
kuishauri namna ya kuboresha matumizi ya ardhi katika kituo hicho.
Baadhi ya wabunge wanaishauri Serikali kuonyesha kujali wagonjwa wa
akili kwa kufanya mkakati wa haraka wa kuhakikisha huduma zinapatikana.
Nchini kuna watu wengi wenye kusumbuliwa na tatizo hilo, mojawapo ya
sababu ikielezwa kuwa msongo wa mawazo na staili za maisha, achilia mbali
historia ya familia na magonjwa mengine.
No comments:
Post a Comment