Rais mpya wa Kenya, Uhuru Kenyatta amefungua rasmi Bunge la nchi yake kwa
kutangaza vita dhidi ya rushwa ambayo imekithiri katika idara nyingi za
Serikali.
Akizungumza kwa kujiamini kwenye Ukumbi wa Bunge uliokarabitiwa hivi
karibuni, Kenyatta alieleza kwamba hivi sasa anaandaa safu ya mawaziri makini
watakaomsaidia kuendesha Serikali yake na watakaohakikisha anatimiza agenda
zake muhimu.
Katika hotuba yake kwa wabunge na maseneta jijini Nairobi, Kenyatta
alisema kwamba suala la rushwa limekuwa kikwazo katika utoaji huduma.
Kenyatta pia alitaja vipaumbele vinane muhimu katika Serikali, ambavyo
ni kuhakikisha kunakuwepo uwazi katika utoaji wa huduma za jamii, kuzalisha
nafasi za ajira, elimu, ulinzi, kuboresha miundombinu na kuwa na Serikali
itakayosaidia kuimarisha umoja wa kitaifa.
“Serikali yangu pia itasimamia sheria ipasavyo ikiwamo kuwasilisha
miswada bungeni na kusimamia utekelezaji wa Katiba Mpya ya nchi hiyo.
“Pia suala la usalama ni muhimu sana, tunatakiwa kuongeza idadi ya
polisi, kuwajengea uwezo wa vifaa na kuboresha masilahi yao,” alisema Kenyatta.
Katika suala la elimu, Kenyatta alisema wanafunzi wote watakaoanza
darasa la kwanza mwaka kesho na wale wanaoingia vyuo vya elimu ya juu
watapatiwa kompyuta pakatwa (laptop).
Hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zake alizotoa wakati wa kampeni
iliyompa ushindi.
Alieleza kwamba vyuo vya elimu ya juu pia vinatakiwa viongezwe kwenye
kaunti zote ili kuzuia vyuo vya elimu ya kati kutumika kama vyuo vikuu.
Katika suala la ajira, Uhuru alieleza kwamba upo umuhimu wa kuwawezesha
vijana na wanawake kupata ajira, mfuko maalumu umeanzishwa, ambapo fedha za
miradi zitatakiwa kupelekwa kwenye ngazi ya majimbo.
Kenyatta alisema kwamba kwa sasa upo umuhimu wa kuangalia zaidi kwenye
mapinduzi ya viwanda na kuhakikisha kwamba wanaandaa na kuboresha bidhaa za
ndani.
No comments:
Post a Comment