Cardiff City imekuwa timu ya kwanza kujihakikishia nafasi ya kupanda
daraja la ligi kuu soka nchini England msimu ujao licha ya sare ya bila
kufungana na Charlton Athletic katika mchezo wa usiku huu.
Pointi moja waliyoipata, iliwatosha kabisa kuwafanya wawe miongoni mwa
timu 20 zitakazo pambana msimu ujao kusaka ubingwa wa kombe la ligi kuu nchini
England,ligi yenye mashabiki wengi duniani.
Hii imekuwa mara ya kwanza kwa Cardiff kurejea kwenye ligi ya juu zaidi
nchini Uingereza baada ya miaka 51 ya kupambana kwenye ligi ndogo toka
waliposhuka daraja mwaka 1962.
Cardiff inakuwa timu ya pili kutoka nchi ya Wales ambayo ni sehemu ya
Taifa la Uingereza kushiriki ligi kuu baada ya Swansea iliyopanda daraja misimu
miwili iliyopita. Pia inakuwa timu ya 46 tofauti kushiriki ligi kuu nchini
England toka ilipoitwa ligi kuu ya England mwaka 1992.
Misimu mitatu iliyopita,Cardiff ilijitahidi kupanda daraja lakini
ilijikuta ikishindwa baada kutolewa kwenye michezo ya mtoano,lakini msimu huu
umekuwa wa mafanikio kwa klabu hiyo ambayo inanolewa na kocha Malcolm George
kutoka Scotland.
Miaka mitatu iliyopita,wiki chache baada ya kufungwa na Blackpool na
kupoteza nafasi ya kwenda ligi kuu,Cardiff ilijikuta kwenye matatizo makubwa
baada ya kufikishwa mahakamani mara tatu baada ya kushindwa kulipa deni la
malimbikizo ya kodi. Lakini deni hilo lilikuja kulipwa lote kwa pamoja na
Bilionea Vincent Tan kupitia kampuni yake ya Malaysian Consortium ya
Malaysia,ambayo iliwekeza kiasi cha paundi milioni 60 kwenye klabu hiyo.
Timu nyingine zitakazopanda daraja msimu ujao kwenye ligi ya Uingereza
na zile zitakazoshuka kutoka ligi kuu kwenda ligi ya chini zitajulikana
mwishoni mwa mwezi ujao
No comments:
Post a Comment