WanaCCM wa Ifakara mjini ‘wamemshtaki’ Katibu Mkuu wa zamani wa CCM,
Yusuph Makamba kwa Katibu Mkuu wa sasa wa chama hicho, Abdulrahman Kinana kwa
ahadi yake aliyoitoa 2008 ya kuwapatia Sh1 milioni ambayo hajaitimiza.
Mwenyekiti wa CCM wa tawi la Ifakara mjini, Felista Chakachaka alisema kwamba
mwaka 2008, Makamba alipotembelea tawi hilo, aliwaahidi kuwapatia Sh1 milioni
kwa ajili ya kazi za tawi hilo lakini hakuitekeleza.
Hata hivyo, Makamba aliyeko Bumbuli mkoani Tanga, alisema jana: “Sawa,
mimi nilitoa ahadi hiyo, sikuitekeleza, sasa aliyepo si ndiyo anatoa...kwani
ahadi za Mwalimu Nyerere si Mzee Ali Hassan Mwinyi kazitekeleza, sawa na ahadi
za Benjamini Mkapa ambazo Rais Jakaya Kikwete anatekeleza.
“Huyu wa sasa aliyepo madarakani ndiye chama, ile ni ahadi ya chama,
ulifikiri Makamba n’toe fedha yangu mfukoni, ile ni ahadi ya chama,” alisema
Makamba.
Akijibu hoja hiyo, Kinana alisema kwa kuwa Makamba aliahidi kiasi hicho
cha fedha akiwa katibu mkuu, basi yeye atatoa fedha hizo. “Katika kipindi cha
wiki mbili fedha hizo zitakuwa zimeingia katika akaunti yenu..nitawapatia kama
alivyoahidi alisema Kinana.
Mbali na kutembelea tawi hilo, Kinana alifungua mashina ya wakereketwa
matano mjini Ifakara.Kinana yuko ziarani mkoani humo kuangalia maendeleo ya
chama hicho tawala.
No comments:
Post a Comment