Mwimbaji nguli wa muziki wa tarabu nchini Tanzania Fatma binti Baraka,
maarufu kama Bi Kidude amefariki Jumatano kisiwani Zanzibar akiwa na umri wa
zaidi ya miaka 100.
Taarifa ya kifo chake ilitolewa na mjukuu wake Fatuma Baraka ambaye pia
ni muimbaji wa Taraabu. Alisema Bi Kidude alifariki hospitalini kutokana na
maradhi ya kisukari na uvimbe kwenye Kongosho.
Bi Kidude amekuwa katika fani ya muziki wa taarab ya kiasili pamoja na
ngoma za unyago kwa zaidi ya robo tatu ya umri wake.
Katika miaka ya karibuni afya yake imekuwa ikizorota kiasi cha serikali
ya Zanzibar kumzuia kupanda majukwaani kuburudisha japokuwa alionekana katika
tamasha la Sauti za Busara mwezi Februari mwaka huu.
Mipango ya mazishi ya nguli huyu inafanywa nyumbani kwake Zanzibar.
Wengi, hasa vijana wa kizazi kipya wanamfahamu Bi. Kidude kwa uwezo
wake mkubwa wa kuimba taarabu kwa kuchanganya lugha ya kiswahili na ile ya
kiarabu. Nyimbo zake za kiarabu mara nyingi zimekuwa na ladha kama ile ya
aliyekuwa mwimbaji gwiji wa Misri Ummu Kulthumu.
Sio uimbaji tu uliomfikisha Bi. Kidude alipofika, bali uwezo wake pia
wa kutunga mashairi, kutumia ala za mziki kama vile kupiga ngoma na hata ngoma
za unyago, vyote hivi vilimuweka Bi. Kidude katika nafasi tofauti katika jamii.
Alikuwa na tabia ya kumwita kila mtu 'mwanangu,' ingawa yeye mwenyewe
hakubahatika kupata mtoto. Katika mahojiano aliyofanyiwa na vyombo mbali mbali
vya habari, mwenyewe alisikika akisema, ingawa alikuwa na hamu ya kupata mtoto,
lakini Mwenyezi Mungu hakumjaalia.
Katika miaka ya hivi karibuni, Bi. Kidude alishirikishwa sana na
wasanii wengine katika kazi zao. Miongoni mwao ni Ahmada Amelewa, Fid Q Juhudi
za Wasiojiweza.
Mbali na hayo, mashirika mbali mbali yakiwemo ya kibiashara na yale
yasiyo ya kiserikali yaliona mvuto aliokuwa nao Bi. Kidude katika jamii, hivyo
wakamtumia katika matangazo mbali mbali maarufu likiwa lile la kutokemeza
Malaria.
Ni bibi aliyebahatika kusafiri takriban duniani kote, na vilevile
katika maisha yake alijinyakulia tuzo lukuki. Miongoni mwa hizo ni ile ya 2005
WOMEX ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa katika tasnia ya muziki.
Katika siku zake za mwisho, Bi. Kidude alikuwa akiumwa, lakini wengi
wanahusisha kuumwa kwake na utu uzima aliokuwa nao.
Kifo chake ni pigo kubwa kwa wote, lakini zaidi ni wanamziki wa kizazi
kipya waliokuwa wakimuona Bi. Kidude ni nyanya yao.
No comments:
Post a Comment