Language

Tuesday, 23 April 2013

MAREKANI YASHINIKIZA MAZUNGUMZO YA AMANI MASHARIKI YA KATI

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry yuko mjini Brussels ambako anatarajiwa kukutana na mkuu wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barosso, na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov. 

Kerry mwishoni mwa wiki alifanya ziara katika Ukingo wa Magharibi katika juhudi za kushinikiza kuanzishwa tena mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina. Bruce Amani ana mengi zaidi
Akiwa mjini Istanbul hapo jana Jumapili, waziri huyo wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry alimtaka Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kuchelewesha ziara yake katika Ukanda wa Gaza mnamo Mei 16 baada ya kuitembelea Ikulu ya Marekani, kwa sababu itahujumu juhudi za kuimarisha mahusiano baina ya Uturuki na Israel.

Israel na Palestina zinapinga ziara hiyo ya Tayyip Ukanda wa Gaza. Wakati akiwa ziarani nchini Israel mwezi uliopita, rais wa Marekani Barack Obama aliwataka viongozi wa Uturuki na Israel kuimarisha mahusiano yao ambayo yalivunjika baada ya shambulizi la 2010 la Israel katika meli ya mizigo iliyokuwa ikielekea Gaza, na kuwauwa Waturuki wanane na Mmarekani mmoja mwenye asili ya Kituruki.
Wapatanishi wa Israel na Uturuki wanapanga kukutana wiki ijayo ili kujadili masharti ya Uturuki ya kulipwa fidia waathiriwa wa mashambulizi hayo ya meli. Kerry alikuwa mjini Istanbul kuhudhuria kongamano la kimataifa kuhusu Syria ambalo lilianza Jumamosi na kuendelea hadi jana Jumapili wakati washiriki wakijadiliana kuhusu namna ya kuimarisha msaada kwa waasi wanaopigana kumwondoa madarakani rais Bashar al-Assad. Alitangaza kuwa Marekani itaongeza maradufu msaada wake usio wa silaha kwa waasi wa Syria pamoja na kiasi cha dola milioni 123 katika vifaa ambavyo huenda vikajumuisha kwa mara ya kwanza magari ya kivita, miwani za kuona usiku miongoni mwa vifa vingine vya kujikinga.
Wakati huo huo, Upinzani nchini Syria umelitaka kundi la wanamgambo la Lebanon la Hezbollah kuwaondoa wapiganaji wake kutoka nchini Syria. Wanaharakati wamesema kuwa majeshi ya serikali yanayoungwa mkono na watu wenye silaha wenye mafungamano na kundi hilo la Hezbollazh jana Jumapili walipambana na waasi kutaka kudhibiti vijiji kadhaa karibu na mpaka wa Lebanon na Syria. Muungano wa upinzani wa Syria, umeonya kuwa kujihusisha kwa Hezbollah katika vita vya Syria kunaweza kusababisha hatari kubwa katika eneo hilo. Wakati huo huo, kiongozi wa muungano huo, Mouaz al-Khatib, jana amewasilisha barua ya kujiuzulu. Taarifa hizo zimetolewa kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa muungano huo wa Facebook.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...