Manchester United imetwaa rasmi ubingwa wa 20 wa taji la ligi kuu
soka nchini England kwa ushindi wa mabao matatu ya aina yake dhidi ya
Aston Villa,Mabao yaliyofungwa kwa ustadi mkubwa na mshambuliaji wa
kimataifa wa Uholanzi Robin Van Persie ambaye sasa atakuwa akiongoza
safu ya wafungaji kwa kufikisha mabao 24 huku Luis Suarez akifuatia
akiwa na mabao 23.
Van
Persie alifunga mabao yote matatu ndani ya dakika 31 za kipindi cha
kwanza katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Old Traford na
kuwafanya United kufikisha pointi tofauti ya 16 na waliokuwa mabingwa
watetezi majirani zao Manchester City,huku wakiwa na michezo minne
kibindoni.
Mkongwe Ryan Giggs alianza kwa kumtengenezea
nafasi ya goli la kwanza Van Persie dakika mbili baada ya mchezo kuanza
kabla ya Wayne Rooney kumpa nafasi nyingine nzuri Van Persie dakika ya
13 na kufunga moja kati ya mabao bora kabisa msimu huu kwa mguu wake wa
kushoto na kufanya United kuwa mbele kwa mabao mawili ndani ya dakika 15
za kwanza za mchezo.
Alikuwa ni Giggs kwa mara nyingine aliyempa
pande Van Persie na kufunga bao la tatu dakika ya 33 ya kipindi cha
kwanza na kufanya uwanja wa Old Traford kulipuka kwa shangwe za
mashabiki,kwani ilikuwa dhahiri wamekwisha jihakikisha ubingwa msimu
huu.
Hii imekuwa mara ya nne kwa Manchester United
kutwaa ubingwa wa ligi kuu soka nchini Uingereza kwenye uwanja wa Old
Traford,baada ya kufanya hivyo mwaka 1999,2002 na 2009. Mara ya mwisho
United kutwaa ubingwa wa ligi kuu huku wakiwa na michezo mingi
iliyosalia ilikuwa mwaka 2001 baada ya kutangazwa mabingwa huku wakiwa
na michezo mitano kibindoni.
Van Persie na Rio Ferdinand wakicheza gangnam kusheherekea ubingwa |
Huu ni ubingwa wa 13 wa taji la ligi kuu ya
Uingereza kwa kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson tangu
alipoanza kuifundisha timu hiyo mwaka 1986.
Kwa matokeo hayo Aston Villa watasalia kwenye
nafasi ya 17 wakiwa na pointi zaidi ya timu ambazo zipo kwenye hatihati
ya kuteremka daraja.
Manchester United wikiendi ijayo watapambana na
Arsenal kwenye uwanja wa Emirates wakati wakisubiri kukabidhiwa kombe
lao la ligi kuu katika mchezo wao mwisho kwenye uwanja wao wa nyumbani
wa Old Traford hapo May 12 watakapokuwa wakicheza na Swansea.
No comments:
Post a Comment