POLISI mkoani Mbeya kwa kushirikiana na polisi mkoani Iringa wamegundua mtandao wa majambazi Sugu ambao umekuwa ukihusika na matukio ya mauaji na unyang’aji wa kutumia silaha.
Kamanda wa polisi mkoani hapa Diwan Athumani amesem leo(Feb 25) kuwa watu 13 wakiwemo askari wawili wanashikiliwa huku wengine 16 wakiendelea kufanyiwa uchunguzi na jeshi hilo. Kamanda Athumani aliwataja askari waliokamatwa kuhusika na mtandao huo kuwa ni MT 85393 Samwel Balumwina(31) wa kikosi cha 844 KJ cha Jeshi la kujenga Taifa(JKT) Mbeya na polisi G 9101 PC Samwel Kigunye(27) wa kikosi cha kutuliza ghasia(FFU) Mbeya. Alisema askari hao wamekuwa wakihusika na mtandao wa ujambazi kwa kuazimisha sare za polisi na jeshi la wananchi(JWTZ) kwa wenzao wanaokwenda katika matukio ya uvamizi na kusisitiza kuwa
watashitakiwa kijeshi. Wengine wanaoshikiliwa ni wanafamilia watatu wote wakazi wa makambako Japhet Ng’ang’ana(24) aliyekuwa mtunza silaha,Claud Ng’ang’ana(36) na mfanyabiashara Hilary Ng’ang’ana(30). Aliwataja wengine kuwa ni Mkazi wa Dar es salaam Rajab Mwinyi(Wakongowe)(25),mkazi wa Sabasaba jijini Mbeya Gregory Mtega(Chambo au Stanley)(25),mkazi wa Tunduma wilayani Momba Francis Sanga(Masalala)(30) aliyekuwa akinunua mali za wizi na mkazi wa Mwanjelwa Gati Mbilinyi ambaye alikuwa akitumia sare za JWTZ katika matukio ya uharifu. Kamanda huyo alisema watuhumiwa hao wote wanaonekana kuhusika na tukio la mauaji ya watu wawili waliotekwa wakati wakitokea dar es salaam kwenda Mbeya kisha kuuawa kwa kupigwa risasi na miili yao kutupwa porini na baadaye kupatikana ikiwa imeoza na kubakia mifupa mitupu maeneo ya Mafinga. Aliwataja watu hao ambao waliuawa Februari 2 mwaka huu na mali waliyokuwa wakisafirisha kuporwa kuwa ni Festo Kyando(45) aliyekuwa dereva na mmiliki wa gari namba T 586AGX Mitsubish Fuso lililokuwa na mzigo wa bidhaa mbalimbali ikiwemo vifaa vya ujenzi pamoja na mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Jamali aliyekuwa utingo. Kamanda Athuman aliwataja wanaoshikiliwa kutokana na mauaji ya askari polisi G.68 PC Jafari Karume Mohamed(30) wa kituo kidogo cha polisi cha Mkwajuni wilayani Chunya katika majibizano ya risasi katika ya majambazi watano na polisi ambapo pia jambazi Shaban Msule(33) mkazi wa Makambako aliuawa. Watuhumiwa hao ni Manase Kibona(Masai)(37) mkazi wa Tunduma na Dar es salaam aliyehusika pia na uporaji katika makazi ya watawa wa kike wa kikatoliki(Masista) huko Wanging’ombe,Mashaka George(27) dereva wa bodaboda aliyekamatwa akiwa amewapakia baadhi ya majambazi katika kijiji cha Kanga wilayani Chunya,Mkazi wa Chimala wilayani Mbarali John Mahenge(39) na Narasco Mabiki(32) mkazi wa Chimala. Alisema pamoja na watuhumiwa hao 13 pia zimekamatwa silaha mbalimbali ikiwamo Bunduki Short Gun moja,bastola tatu,gobore moja,risasi 155 za aina mbalimbali za bunduki,magari manne mali ya watuhumiwa wa mtandao huo na sare nne za JWTZ. Alisema mtandao huo umekuwa ukifanya matukio ya unyang'anyi wa mali na mauaji katika mikoa ya Mbeya,Iringa na Morogogo katika maeneo ambayo yamekuwa yakitajwa kushamiri kwa utekaji magari.
No comments:
Post a Comment