Language

Thursday, 25 April 2013

UNAMFAHAMU ALIYEBUNI JINA LA TANZANIA? MSOME HAPA


HISTORIA ya Tanzania haiwezi kukamilika bila kutaja jina la mtu maarufu aliyebuni jina la Tanzania ambaye kwa bahati mbaya au kwa makusudi hakumbukwi tena.


Tunaelezwa kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lakini nani kati yetu amekuwa akijiuliza jina la Tanzania lilivyopatikana na nani hasa alilibuni?
Wengi tunaambiwa kuwa jina la Tanzania lilipendekezwa na Watanganyika, Wazanzibari na raia wengine wa nje lakini hawatajwi waziwazi na picha zao tukaziona.
Inaaminika kuwa mtu aliyebuni jina la Tanzania ni MOHAMMED IQBAL DAR, raia wa India ambaye alikuwa miongoni mwa watu walioshindana katika shindano la kubuni jina la nchi mpya baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana.
Mohammed alizaliwa mkoani Tanga miaka ya 1944; baba mzazi wa Mohammed alikuwa daktari huko mkoani Morogoro akiitwa Dk. T . A DAR aliyefika Tanganyika kuanzia mwaka 1930.
Mohammed Iqbal Dar alipata elimu yake ya msingi mkoani Morogoro katika Shule ya Msingi H. H D Agakhan ambayo kwa sasa ni mali ya serikali. Alijiunga na Shule ya Sekondari Mzumbe alikosoma kidato cha kwanza hadi cha sita.

Aliingiaje kwenye shindano la kupendekeza jina la Muungano kati Tanganyika na Zanzibar?
Mohammed anasema alikuwa maktaba akisoma gazeti la Tanganyika Standard (siku hizi Daily News) akaona tangazo lililowataka wananchi washiriki shindano la kupendekeza jina moja ambalo lingezitaja nchi zote mbili yaani Tanganyika na Zanzibar.
Mohammed Iqbal Dar anasema aliamua kuingia kwenye shindano. Kwanza alichukua karatasi akaandika Bismillah Rahman Rahim, hii ni kutokana na imani yake.
Kisha akaandika jina la Tanganyika na kufuatia Zanzibar. Aliandika jina lake Iqbal, halafu jina la jumuia yake ya Ahmadiya.
Iqbal Dar alichukua herufi tatu kutoka Tanganyika yaani TAN na kwa upande wa Zanzibar akachukua herufi tatu za mwanzo ZAN na kuziunganisha akapata neno TANZAN.
Anadai alijaribu kutafakari na kuona nchi nyingi za Afrika ziliishia na majina ya IA, kama vile Zambia, Tunisia, Namibia, Gambia, Nigeria n.k, hivyo akaamua kuchukua herufi ya kwanza ya jina lake Iqbal na akachukua herufi A kutoka jina la dini yake ya Ahmadiyya na kuziunganisha na akapata jina kamili la TANZANIA, likiwa limezaliwa kutoka majina ya Tanganyika, Zanzibar, Iqbal na Ahmadiyya.
Mohammed Iqbal Dar alituma jina hilo kwenye kamati ya kuratibu shindano, ambapo baada ya muda alipokea barua nzito kutoka serikalini na kusainiwa na Idrisa Abdul Wakil ambaye alikuwa Waziri wa Habari na Utalii wa wakati huo ikimjulisha kuwa alikuwa miongoni mwa washindi katika shindano hilo.
“Utakumbuka kuwa miezi michache iliyopita ulituandikia kutupa ushauri kuhusu jina jipya la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na wewe pamoja na wananchi wenzio 16 ulishauri nchi yetu iitwe Tanzania.
“Nafurahi kukuarifu kuwa mshirikiane ile zawadi ya sh 200 iliyoahidiwa na leo nakuletea check ya sh 12/50 ikiwa ni hisa yako katika zile sh 200. Nashukuru sana kwa jitihada ya kufikiri jina la jamhuri yetu,” ilisema barua hiyo.
Sasa kwa nini Mohamed Iqbal Dar anadai kuwa mshindi pekee wakati barua ilionyesha kulikuwa na washindi wengine 15? Anasema wakati wa kutolewa kwa zawadi hizo hakuna aliyejitokeza zaidi ya Mohammed Iqbal Dar na Yusufal Pir Mohamed ambaye hata hivyo alikosa sifa baada ya kushindwa kutoa barua ya pongezi ya kushinda kwa madai kuwa ameipoteza.
Hivyo Wizara ya Habari na Utalii iliamua kumtangaza Iqbal Dar kuwa mshindi na kumpatia zawadi yote ya sh 200 pamoja na ngao.
Iqbal Dar anayo masikitiko ya mchango wake kutotambuliwa ingawa anaipenda Tanzania na anajivunia kuwa Mtanzania japo ana asili ya India.
Mohammed Iqbal Dar kwa sasa anaishi Uingereza kwa kuwa huko ndiko alikopata kazi eneo la Birmigham b35 6ps UK, Dar –es-Salaam House, 18 TURNHOUSE ROAD,PHONE 44 121-747-9822

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...