Language

Friday, 12 April 2013

UHURU KENYATTA: "SIKU 100 ZINANITOSHA KUTIMIZA AHADI ZANGU ZOTE"



Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema kwamba atatumia siku 100 tu  kutekeleza ahadi  zake zote ambazo ameziahidi kipindi cha kampeni.

Alisema  kwanza atatumia miezi mitatu tu kuondoa kabisa malipo ya Afya ya uzazi kwa kina mama katika zahanati zote na hospitali za umma.
Alisema kwamba Serikali yake itatoa kiasi cha Sh6 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mfuko wa vijana na wanawake .
Pia alikumbushia ahadi ya kutoa ‘laptop’ kwa wanafunzi wote wa shule za msingi watakaojiunga na shule za serikali mwakani.
Uhuru alisema kwamba kutekeleza ahadi hizo ni katika suala la utekelezaji wa sera  na misimamo wa Muungano wa Jubilee.

“Mimi nina fahari kubwa kuwajali wanyonge waliokubali kunipa nafasi hii ya uongozi na nimekubali kulivaa vazi hili la uongozi hivyo nitasimamia sera za Jubilee kama tulivyoahidi Wakenya wakati wa kampeni,’’ alisema Uhuru.
Aliongeza kwamba yupo kwa ajili ya Wakenya wote waliompigia kura  na hata wale waliowapigia wapinzani wake.
Uhuru alisema atawasaidia Wakenya pamoja na taifa zima kuelekea katika mizizi imara ya kiutajiri kwa njia ya amani, hali ambayo alisema inawezekana ikafanikiwa kwa kiasi kikubwa baadaye.
Naye mtaalamu wa Uhusiano wa Kimataifa, Profesa Munene Macharia alipokuwa akifanya mahojiano na Kituo cha Habari cha Xinhua ,alisema kwamba kuchaguliwa kwa Rais Uhuru Kenyatta, kuna uwezekano mkubwa kubadilika kwa sera za kiuchumi.
Alisema kwamba Rais huyo ambaye awali alikuwa   katika Baraza la Mawaziri  la awamu iliyopita akiwa Waziri wa Fedha anatakiwa kujenga uhusiano wa karibu na mataifa ya nje ili aweze  kubadili sera za kiuchumi.
Pia alimtaka waziri huyo kuangalia suala la  kuimarisha uhusiano wa kibiashara na nchi jirani za Afrika na  Afrika Mashariki.
Profesa Macharia alisema baada ya kuitumikia Serikali ya Kibaki, Kenyatta ana uwezo mkubwa  wa kudumisha sera hiyo ya kiuchumi.
“Lengo la msingi kwa Serikali ya Kenyatta inatakiwa kuimarisha mahusiano yake na Jumuiya ya Afrika Mashariki nchi wanachama (EAC) Kama majirani wa karibu,” Macharia alibainisha.
Wakati huohuo Rais  mstaafu Mwai Kibaki aliwahakikishia raia wa Wakenya kuwa, wapo katika mikono salama baada ya yeye kustaafu rasmi juzi.
Alisema kwamba yeye anaanza maisha yake ya kustaafu, hivyo raia wote wa nchi hiyo wanatakiwa kufahamu kwamba wanabaki katika mikono salama wasiwe hivyo wasiwe na hofu yoyote ile.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...