Muungano wa Cord umeeleza kwamba unaendelea kukusanya ushahidi wa
malalamiko yao ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi mgombea wa
Muungano wa Jubilee na utayafikisha kwenye Mahakama ya Rufaa Jumatatu wiki
ijayo.
Waziri wa Elimu, Mutula Kilonzo alisema kwamba muungano wao wa Cord uliomsimamisha Waziri Mkuu Raila Odinga ambaye ameshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Machi 4 umekuwa ukiendelea kukusanya taarifa na maelezo ya ushahidi kutoka vyanzo mbalimbali.
“Tumeomba taarifa kutoka kwa taasisi kadhaa ambazo ni muhimu katika kukamilisha mkakati huu,” alisema.
Kilonzo alionya kwamba shamrashamra za awali za ushindi zi nazoendelea katika maeneo mengi zitabadilishwa na uamuzi wao mara tu watakapokamilisha kukusanya ushahidi na kufungua rasmi kesi mahakamani.
Msimamo huo umetolewa jana, baada ya Jaji Mkuu Dk Willy Mutunga kueleza kwamba yuko tayari kupokea na kuyatolea uamuzi malalamiko yote yanayohusiana na uchaguzi, ikiwamo pingamizi la matokeo ya urais lililokuwa limetarajiwa kuwasilishwa jana.
Mutunga alisema Mahakama ya Rufaa itahakikisha inashughulikia vyema malalamiko hayo na kutoa uamuzi sahihi ndani ya muda uliowekwa na Katiba ya nchi chini ya Majaji sita wa Mahakama ya Rufaa.
Pia aliviomba vyombo vya habari kuwapo mahakani hapo ili kuripoti moja kwa moja mwenendo mzima wa usikilizwaji wa shauri hilo na kuufanya umma kupata picha halisi ya kile kitakachokuwa kikifanyika.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Ardhi, James Orengo alisema kwamba Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) ilitangaza matokeo ya uchaguzi ziku ya Jumamosi ambayo kimsingi siyo siku ya kazi hivyo Cord inatarajia kufungua rasmi kesi yake Jumatatu ijayo.
Pia aliituhumu IEBC akisema kwamba imekuwa ikishikilia kwa makusudi baadhi ya nyaraka muhimu ili kuiyumbisha Cord katika kukusanya matokeo halisi ya kura.
“Tumekuwa tukinyimwa haki ya kupitia nyaraka muhimu zilizoko chini ya IEBC. Hivyo inatufanya tushindwe kupata kwa wakati baadhi ya nyaraka muhimu katika ushahidi,” alisema Orengo
No comments:
Post a Comment