Takriban watu 260,000 walifariki dunia wakati wa ukame ulioikumba Somalia
kuanzia mwaka 2010 hadi 2012, utafiti umebaini.
Nusu ya waliofariki dunia walikuwa ni watoto wenye umri chini ya miaka
mitano, inaeleza ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo,
FAO, pamoja Mtandao wa Kuonya Mapema Kuhusu Majanga ya Ukame unaofadhiliwa na
Marekani.
Idadi ya vifo ilikuwa kubwa kuliko ile iliyokadiriwa ya watu 220,000
waliofariki wakati wa ukame wa mwaka 1992.
Janga hilo lilisababishwa na ukame mkali, uliochochewa na mapigano kati
ya makundi hasimu yaliyokuwa yakigombea madaraka.
Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza ulitangaza hali ya ukame Julai 2011
katika mikoa ya Somalia ya Bakool uliopo kusini na ule wa chini wa Shabelle,
ambayo ilikuwa inadhibitiwa na kundi la wanamgambo wa Al – Shabab wenye
mafungamano na Al – Qaeda.
Lakini kundi hilo lilikanusha kuwepo kwa hali hiyo na kuyapiga marufuku
mashirika kadhaa ya misaada ya nchi za magharibi kufanya shughuli zake katika
maeneo hayo.