Abiria saba waliokuwa wakisafiri na basi la kampuni ya Taqwa lenye namba
za usajili T 273 CDR kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Malawi wamekufa papo
hapo na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa vibaya katika ajali iliyotokea jioni jana katika eneo la Nyololo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Mmoja kati ya mashuhuda aliyejitambulisha
kwa jina la Dkt Matatala alisema kuwa ajali hiyo imetokea JANA mida ya saa 11
jioni wakati basi hilo likitokea Dar es Salaam kwenda
nchini Malawi.
Alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni lori
lenye namba za usajili T 104 DZZ ambalo lilikuwa likitokea Makambako kuelekea
Iringa,lori lililokuwa likijaribu kulipita lori lenye namba za usajili T 227
AVC na kushindwa kupita na kuishia kugongana uso kwa uso na basi hilo ambalo
pia lilikuwa likija kwa mwendo wa kasi.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo
wamesema kuwa ajali hiyo imetokea katikati ya mji wa Nyololo ambapo ni jirani
kabisa na eneo lenye matuta ya kuzuia magari kwenda kwa mwendo kasi.
Alisema kuwa hadi majira ya saa 12.45 jioni maiti tano zilikuwa
zimetolewa katika basi hilo la Taqwa na kuwa jitihada za wasamaria wema kutoa
maiti na majeruhi katika eneo hilo zimeendelea kufanyika.
Mbali ya maiti hizo pia alisema jumla ya majeruhi 20 waliokolewa na
kukimbizwa katika Hospitali ya wilaya ya Mufindi kwa matibabu zaidi. Dkt
Matatala alisema kuwa katika tukio hilo wananchi wameweza kuimarisha ulinzi
zaidi katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kulinda mali za majeruhi na abiria
waliopoteza maisha yao kwa ajili hiyo.
Wakati huo huo wananchi wa eneo hilo la Nyololo wameelekeza lawama zao
kwa jeshi la polisi wilayani Mufindi kwa kuchelewa kufika katika eneo la tukio
na kuwa taarifa wamepewa mapema ila hadi majira ya saa 12.50 hakukuwepo na
askari aliyefika eneo hilo.
Hii ni ajali ya pili kutokea katika wilaya ya Mufindi kwa kipindi cha
wiki moja baada ya ajali nyingine mbaya kama hii kutokea eneo la Mafinga kwa
gari ndogo iliyokuwa ikiendeshwa na paroko wa kanisa katoliki Ifunda marehemu
Alfonce Mhamilawa kutokea kwa kuingia nyuma ya lori.
No comments:
Post a Comment