Vurugu kubwa zilizuka jana katika Mji wa Tunduma ambao ni makao makuu ya
Wilaya ya Momba, Mkoa wa Mbeya, baada kutokea mvutano mkali kuhusu nani
anayepaswa kuchinja mifugo baina ya waumini wa dini mbili; Waislamu na
Wakristo.
Mamia ya polisi kutoka wilaya zinazouzunguka Mji wa Tunduma walimwagwa na walilazimika kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha ili kuwatawanya waandamanaji pia, kutuliza vurugu zilizodumu kwa zaidi ya saa nne.
Vurugu hizo ambazo zinahatarisha amani, zimetokea siku tatu tu tangu
Rais Jakaya Kikwete aonye kwamba kwamba vurugu zenye sura ya kidini ni hatari
na zinaweza kuvuruga amani na utulivu uliodumu kwa miaka mingi nchini.
Mijadala kuhusu vurugu hizo ilitawala katika mitandao ya kijamii ikiwamo facebook,
Mabadiliko Forum na Jamii Forums ambako watu mbalimbali walionyesha kukerwa
nazo, huku wakiitaka Serikali ichukue hatua za kudhibiti.
Kutokana na vurugu hizo zilizoanza saa 4:30 asubuhi, wakazi wa mji huo
walijifungia ndani kwa kuhofia usalama wa maisha yao, huku maduka na shughuli
za biashara nazo zikifungwa.
Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwa katika eneo la tukio anaripoti kwamba katika vurugu hizo, watu zaidi ya 35 wamekamatwa wakiwamo Diwani wa Kata ya Tunduma Frank Mwakajoka na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Gidion Mwamafupa.
Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwa katika eneo la tukio anaripoti kwamba katika vurugu hizo, watu zaidi ya 35 wamekamatwa wakiwamo Diwani wa Kata ya Tunduma Frank Mwakajoka na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Gidion Mwamafupa.
Habari zaidi zinasema barabara za mji huo zilifungwa, umeme ulizimika baada ya
moto kulipuka kwenye moja ya nguzo za umeme. Pia mpaka wa Tanzania na Zambia
ulifungwa kwa muda.
Magari ya abiria na yale ya usafirishaji yaliyokuwa yakitoka na kuelekea
Zambia, Dar es Salaam, Sumbawanga na Mbeya Mjini pia yalikwama na kusababisha
usumbufu mkubwa kwa abiria. Msikiti ulivunjwa na watu wawili akiwamo askari
polisi walijeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman alithibitisha kutokea kwa
vurugu hizo na kwamba tukio hilo limetokea wakati Serikali ikiwa kwenye
mazungumzo na baadhi ya wahusika katika mgogoro wakiwamo viongozi wa dini na
wachinjaji wa nyama.
“Mgogoro wa kuchinja umedumu kwa siku tatu, jana kamati ya ulinzi na usalama
chini ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro ilikutana na baadhi ya viongozi
wa dini na wadau wa kuchinja nyama na kuna mambo matatu ambayo yalitolewa
katika mkutano huo,” alisema Diwani.
Alisema katika mkutano huo Kandoro aliagiza kuwa wananchi wanatakiwa kuwa
wavumilivu katika kipindi hiki, ambacho Serikali ngazi ya kitaifa
inalishughulikia na kuwataka kuendelea na hali uchinjaji kama ilivyokuwa awali
na kila mmoja afanye kile anachoamini katika dini yake wakati wa kula.
Hata hivyo, baadhi ya Wakristo waliafikia lakini wengine hawakuafiki. Hivyo
jana asubuhi walihamasisha maandamano katika mji huo ambayo yalisababisha
vurugu hizo.
“Pamoja na hayo yote uchunguzi wa kitaalamu tumebaini kuwa vurugu hizo siyo za
kidini, bali zimehusishwa siasa kwani hata viongozi wa dini waliohusika ni
baadhi siyo wote ambao wanajishughulisha na suala hili,” alisema Diwani.
No comments:
Post a Comment