Language

Saturday, 26 January 2013

BURUDANI:BADO UTATA UMETAWALA!!!

TASNIA ya sanaa ni nyanja ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa ikitawaliwa na amani, huku watu wake wakionekana kuwa na furaha na kufanya kazi zao kwa kujitolea zaidi licha ya mapato kiduchu kutokana na kazi zao.

Hata hivyo, kwa takribani
mwezi mmoja sasa imekuwa ni mshikemshike. Amani inaanza kutoweka taratibu, huku Wizara ya Habari Vijana, Utamaduni na Michezo ikiwa imelifumbia macho suala hili.
Desemba 28, Naibu Waziri, Amos Makalla katika mkutano wake na wasanii ofisini kwake, alijadili kuhusu urasimishaji wa kazi za wasanii ambao ulianza Januari Mosi mwaka huu. Lakini licha ya hilo yapo mengi yaliyojadiliwa ndani yake ikiwa ni pamoja na wizi unaoendelea kufanywa na maharamia wanaojihusisha na kazi za wasanii.
Katika majadala huo kuna baadhi ya wasanii walieleza wazi tatizo hilo, huku wakiwatuhumu baadhi ya viongozi wakubwa wanaoaminiwa kuwalinda wasanii, ambao nao pia walikuwapo katika kikao kile.
Jacob Steven JB, Vicent Kigosi Ray na Bahati Bukuku ni baadhi ya wasanii ambao walitoa dukuduku zao mbele ya Naibu Waziri, huku wakimtuhumu Mtendaji wa Cosota Yustus Mkinga aliyekuwapo katika kikao kile na Makatibu wa Wizara na watendaji wengine wakishuhudia hilo.
Wasanii walitoa ya moyoni, ambayo hata hivyo wizara iliahidi kuyashughulikia lakini hakuna hatua iliyochukuliwa licha ya mhusika kukaa kimya.
Wasanii waliamini kuwa wangesikilizwa na mhusika angewekwa chini na kuulizwa. Januari ilifika na wasanii wakaendelea na kazi zao kama kawaida.
Wasanii hawakupata majibu kwa muda mwafaka. Waliandika barua nyingine, lakini bila kupata majibu hivyo wakaamua kuitisha kikao chao na waandishi wa habari Januari 20 na kuelezea dukuduku lao kabla ya kuamua kuandamana nchi nzima. Ingawa inafahamika kuwa wasanii wa filamu na michezo ya kuigiza wameshauriwa kuzisoma nyaraka mbalimbali za Bodi ya Filamu ili wajue sheria na kanuni zinazohusu tasnia hiyo, wao wamedai kuwa zimekuwa zikiwanyonya sana.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Joyce Fissoo aliwahi kutoa ufafanuzi juu ya Sheria namba 4 ya Utengenezaji wa Filamu na Michezo ya Kuigiza ya mwaka 1976.
Fissoo alisema sheria hiyo ndiyo inayoendelea kutumika hadi sasa na kukanusha taarifa zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu uwepo wa matumizi ya sheria mpya.
Alisema hakuna sheria mpya ya Filamu na Michezo ya Kuigiza iliyotungwa, Sheria inayoendelea kutumika ni ile ya mwaka 1976, bali kilichofanyika ni utekelezaji wa kanuni za sheria ya filamu na michezo ya kuigiza, ambapo mchakato wake ulianza mwaka 2011.
Aliwahi pia kuzungumzia kuhusu malalamiko ya baadhi ya wasanii kushindwa kuhimili kulipa ada ya Sh500,000, Fissoo alisema kifungu cha 8 cha sheria hiyo kinampa mamlaka waziri mwenye dhamana husika kutoa msamaha wa malipo kwa msanii mchanga atakayeshindwa kulipa kiasi hicho cha fedha.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...