Mwanajeshi mmoja nchini Uganda anadaiwa kuwapiga risasi na kuwauwa watu
11 wakiwemo wenzake watatu baada ya mzozo katika baa moja nchini humo.
Polisi walisema wanamsaka mtuhumiwa wa mauaji hayo, ambayo yalitokea
katika maeneo mawili tofauti juzi, huko Entebbe kwenye Wilaya ya Wakiso na
kambi ya jeshi ya Bombo iliyopo kwenye Wilaya ya Luweero.
Polisi imesema kisa hicho kimetokea katika baa iliyoko kwenye soko moja
mjini Bombo kilomita 30 kutoka mji mkuu Kampala, ambapo watu 10 waliuawa papo
hapo huku mmiliki wa baa hiyo ijulikanayo kama Four Turkeys akipigwa risasi
kwenye lango la kuingilia na baadaye kufariki dunia akiwa hospitali.
Akizungumza na mjini Kampala, naibu msemaji wa Polisi wa Uganda, Judith
Nabakooba, alithibitisha kisa hicho na kusema kwamba kwa sasa wanaendelea na
uchunguzi kujua sababu ya mauaji hayo. Nabakooba alisema huenda hali hiyo ikawa
imechochewa na kutoelewana.
“Wataalamu wetu wanatafuta silaha iliyotumika katika mauaji hayo na
baada ya kuipata ndipo tutakapopata mwanga kuhusu muuaji,” alisema.
Wakazi wa eneo hilo walisema kwamba mtu huyo anayedhaniwa kuwa ni
askari aliingia katika baa hiyo wakati kiza kilipoanza kuingia na kufyatua
risasi mfululizo kisha kutoweka.
Hata hivyo, visa vya mauaji kama haya vinavyowahusisha wanajeshi na
polisi walevi si vigeni nchini Uganda.
No comments:
Post a Comment