Language

Tuesday, 22 January 2013

BURUDANI: LULU AOMBA DHAMANA KWA MAHAKAMA KUU

Staa wa filamu Bongo (Bongo Movie), Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia ameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imwachie huru kwa dhamana.
Lulu kupitia kwa wakili wake aliwasilisha ombi hilo Mahakama Kuu ya Tanzania na Ijumaa jaji anayeisikiliza kesi hiyo anatarajia kutoa uamuzi.
Tangu kilipotokea kifo cha msanii, Steven Kanumba, Aprili 7, mwaka jana Lulu
amekuwa akisota mahabusu na dhamana yake ikawa imezuiwa kwa mujibu wa kesi za mauaji.
Hata hivyo baada ya kukamilika kwa upelelezi, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alimbadilishia mashtaka na kuwa ya kuua bila kukusudia hivyo kumuweka katika mazingira ya kupatiwa dhamana. Habari zilizopatikana mahakamani hapo jana zilisema kuwa tayari maombi hayo ya dhamana yamepangwa kusikilizwa na Jaji Zainabu Muruke, Januari 25 ,2013.
Maombi hayo yamewasilishwa chini ya hati ya dharura wakiomba yasikilizwe na kuamuriwa mapema kwa madai kuwa mshtakiwa amekaa rumande kwa muda wa miezi saba na kwamba kosa lake linadhaminika.
Katika hati ya maombi iliyoambatanishwa na hati ya kiapo cha wakili Kibatala kwa niaba ya mshtakiwa huyo, wanaiomba mahakama iamuru mshtakiwa apewe dhamana, akiwa au bila kuwa na wadhamini, au kwa amri na masharti mengineyo ambayo mahakama itaona yanafaa.
Hati hiyo ya maombi ya dhamana inasema, “Kwamba tunaomba Mahakama hii tukufu impe dhamana mshtakiwa akiwa na au bila kuwa na wadhamini, wakati akisubiri usikilizwaji na uamuzi wa kesi yake ya msingi, shauri la jinai namba 125 la 2012, iliyoko katika mahakama hii tukufu.
Alidai kuwa akiwa wakili wa mwombaji, anatambua kuwa mwombaji anao wadhamini wa kuaminika ambao wako tayari kufika mahakamani kama wadhamini kwa niaba yake.
Wakili Kibatala katika hati yake hiyo ya kiapo anadai kuwa akiwa wakili wa mshtakiwa, ikiwa mshtakiwa huyo atakubaliwa dhamana, yuko tayari na ataweza kutimiza masharti yote ya dhamana yatakayotolewa na mahakama.
Aliendelea kudai kwamba kwa muda ambao ameiendesha kesi hiyo amepata fursa kubwa ya kufahamiana na mwombaji pamoja na familia yake na kwamba kwa msingi huo anajua kuwa mwombaji huyo ana tabia nzuri na ni wa kuaminika.
Mwombaji bado yuko chini ya uangalizi wa wazazi wake ambao wako tayari kuhakikisha kuwa anatimiza masharti na kuhakikisha kuwa anafika mahakamani wakati wowote kadri atakavyohitajika kwa ajili ya usikilizwaji wa shauri lake au kusudi lolote’, alisema.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...