HALI si shwari tena katika Kanisa la Moravian Jimbo la Misheni
Mashariki kutokana na Mwenyekiti aliyesimamishwa uongozi na Mkutano Mkuu
wa Jimbo (Sidodi), Mchungaji Clement Fumbo kujichukulia madaraka na
kutangaza uongozi wake mpya.
Fumbo alitangaza uongozi huo juzi katika ibada
iliyofanyika katika Kanisa la Moravian Ushirika wa Tabata akieleza kuwa
uongozi wa juu wa kanisa unamtambua kuwa yeye ndiye mwenyekiti wa kanisa
katika jimbo hilo la Misheni.
Wakati hayo yakijiri sintofahamu imebakia kwa
waumini kuwa hivi sasa waufuate uongozi upi wa mwenyekiti
aliyesimamishwa na sinodi ama Makamu Mwenyekiti Sauli Kajura aliyepewa
mamlaka ya kuliongoza jimbo hadi kipindi cha mkutano mkuu wa uchaguzi
utakaofanyika mwaka 2014.
Kutangazwa kwa uongozi huo wa kanisa kumejiri
wakati pia kesi ikiendelea katika Mahakama ya Kisutu ambapo Mchungaji
Fumbo alifungua kesi ya kupinga uamuzi wa Sinodi akieleza kuwa
hakuhusika na upotevu wa Sh 500m hali iliyosababisha avuliwe uongozi huo
kupitia sinodi ya dharura.
No comments:
Post a Comment