IMEBAINIKA kuwapo kwa wizi wa kutisha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, huku magari ya Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji yakitajwa kwamba yamekuwa yakivusha vifaa vya wizi kutoka ndani ya uwanja huo.
Wizi huo ambao umewasababishia hasara kubwa baadhi
ya wasafiri wakiwamo wafanyabiashara, abiria wa kawaida na watalii
wanaoingia nchini, unadaiwa kufanywa na baadhi ya wafanyakazi wa Wakala
wa Mizigo wa Kampuni ya Swissport.
Wafanyakazi hao wamekuwa wakiiba vifaa na bidhaa
kwa kuchana mabegi ya abiria kisha kuviweka kwenye makoti yao ya kazi
lakini kwa mizigo mikubwa, wamekuwa wakiificha kwenye magari ya zimamoto
ambayo huingia na kutoka ndani ya uwanja wa ndege bila kufanyiwa
ukaguzi.
Chanzo kingine cha habari katika uwanja huo
kinasema magari ya zimamoto yanayofanya kazi katika uwanja huo
hayakaguliwi yanapopita kwenye lango kuu, hivyo kutoa mwanya wa kuvushwa
kwa mali za wizi.
“Mali zinazowekwa katika magari hayo ni zile kubwa
ambazo hutakiwa kuuzwa nje ya uwanja wa ndege kama kontena la simu au
mabegi makubwa ya nguo,” kilisema chanzo hicho.
Baadhi ya waathirika wa wizi huo waliliambia
gazeti hili kwamba wamepoteza mizigo mingi kwa nyakati tofauti na kupata
hasara kubwa na kwamba uwanja huo si salama kwa wafanyabiashara hasa
wanaoingiza bidhaa zao kutoka nje ya nchi.
Chanzo chetu katika uwanja huo kilidokeza kuwa
mara nyingi wizi hufanyika wakati mizigo inaposhushwa kutoka kwenye
ndege kupelekwa eneo la kusubiri kuchukuliwa na abiria pia wakati mizigo
mingine inapohifadhiwa kwenye stoo uwanjani hapo ikisubiri wahusika
kuichukua.
“Wakati wanashusha mizigo kutoka kwenye ndege
wanaikata kwa visu au viwembe vikali na kuchomoa chochote kilichomo
kisha wanaweka katika makoti ya kazi ambayo yana mifuko mikubwa,”
kilieleza chanzo hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Swissport Tanzania,
Gaudence Temu alikiri kuwapo kwa tatizo hilo lakini akasema kampuni yake
kwa kushirikiana na wadau wengine uwanjani hapo wamekuwa wakichukua
hatua za kudhibiti wizi huo.
“Huu wizi unaharibu sifa ya uwanja wa ndege wa
kimataifa, ndiyo maana tukasema hatutakuwa na uvumilivu hata kidogo kwa
wale ambao tunabaini kwamba wanafanya vitendo hivyo,” alisema Temu.
Kamishna Msaidizi wa Zimamoto na Uokoaji, Sikiri
Sala alisema amekwishazungumza na Kikosi cha Zimamoto Uwanja wa Ndege
kuhusu suala hilo ambalo hata hivyo, alisema ni zito na linahitaji
ushirikishwaji wa viongozi wote kwa kuwa uwanja huo una mashirika mengi.
“Wadau wengi wanapaswa kuzungumzia suala hili.
Kuna polisi wa usalama uwanja wa ndege, kuna watu wa usalama, TAA
(Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania) na kampuni za mizigo kama
Swissport. Hawa wote wanatakiwa kufahamu suala hili kwa sababu lina
uzito,” alisema Sala.
No comments:
Post a Comment