Mahakama ya juu zaidi nchini Kenya, imeamua kuwa rais mteule Uhuru
Kenyatta atasalia kuwa rais mpya wa Kenya baada ya kusema kuwa uchaguzi
ulifanywa kwa njia huru na ya haki.
Uchaguzi wenyewe ulifanyika tarehe nne mwezi Machi, ambapo hesabu ya
kura ilimpa ushindi Kenyatta kwa zaidi ya laki nane.
Rais wa mahakama hiyo jaji mkuu Willy Mutunga alisema kuwa mahakama
imekubali kwa kauli moja kuwa uchaguzi ulifanywa kwa njia ya huru na wazi na
kuwa Kenyatta na mgombea mwenza wake walichaguliwa kihalali.
Uamuzi huu una maana kuwa Uhuru Kenyatta ndiye ataapishwa kama rais
mpya wa Kenya tarehe tisa mwezi ujao
Kesi hiyo iliwasilishwa katika mahakama ya juu zaidi na mpinzani mkuu
wa Kenyatta, Raila Odinga baada ya uchaguzi uliofanyika mapema mwezi huu.
Matokeo rasmi yalionyesha kuwa Uhuru alishinda uchaguzi kwa kumpiku
Raila kwa asilimia 50.07 huku Raila akipata asilimia 43.28. Matokeo haya
yalizuia kufanyika kwa duuru ya pili ya uchaguzi kwa kura 8,100.
Bwana Odinga aliishutumu tume huru ya uchaguzi na mipaka kwa kuhujumu
matokeo ya uchaguzi ili kumpa ushindi Uhuru Kenyatta.
Uchaguzi wa urais, wabunge na wajumbe wengine wa serikali, ulifanyika
tarehe nne mwezi Machi, ukiwa wa kwanza tangu uchaguzi uliokumbwa na ghasia
mwaka 2007 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya elfu moja.
Bwana Kenyatta na mgombea mwenza wake ,William Ruto,wanakabiliwa na
kesi katika mahakama ya jinai kwa kuchochea ghasia za mwaka 2007. Hata hivyo
wamekanusha vikali mashtaka.
Mahakama ya juu zaidi inaweza kuthibitisha ushindi wa Kenyatta au
kuubatilisha uamuzi wa wakenya na hivyo kuitisha uchaguzi mpya.
Vyovyote matokeo yatakavyokuwa kuna wale watakaoghadhabika mno.
Rais anayeondoka mamlakani, Mwai Kibaki amewataka wakenya kuwa watulivu
na kukubali uamuzi wa mahakama lakini wengi wanatagemea sana idara ya mahakama
ambayo imekuwa na mageuzi makubwa na ambayo sasa watu watu imani nayo.
Mawakili wa Odinga wanasema kuwa kesi yao ilihusisha madai ya kuhujumu
hesabu ya kura pamoja na matatizo ya usajili wa wapiga kura na vile vile
matatizo ya mitambo ya usajili wa wapiga kura.
Mnamo Ijumaa mahakama ya juu zaidi ilidurusu matokeo ya kura katika
vituo 22 vya kupigia kura. Na pande zote mbili zilisema matokeo yalithibitisha
misimamo yao.
Kenyatta ameutaja uchaguzi huo kama ishara ya kukuwa kwa demokrasia
Kenya na ulifanywa kwa njia ya amani.
Tume ya uchaguzi, pia imesisitiza kuwa uchaguzi ulikuwa huru licha ya
hitilafu za kimitambo
Wachunguzi wa kimataifa nao walisema kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa
haki na kuwa tume huru ya uchaguzi uliendesha uchaguzi huo kwa uwazi.
No comments:
Post a Comment