BAADHI ya mastaa wa kikosi cha kwanza, Simba (majina tunayo) wamesema
hawana imani na mbinu za Kocha Mkuu Patrick Liewig na hilo limethibitika zaidi
katika mchezo wao wa Angola.
Mwishoni mwa wiki, Simba ilishambuliwa na kipigo cha mabao 4-0
kutoka Recreativo Libolo ya Angola katika mchezo wa marudiano Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kuaga mashindano raundi ya kwanza kwa
jumla ya mabao 5-1, kutokana na kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wiki
mbili zilizopita, Dar es Salaam.
Wakizungumza juzi usiku kwenye hoteli ya Ritz iliyopo mji wa Calulu
lilikofanyika pambano hilo la marudiano, mastaa hao wamesema mfumo wa sasa wa
Simba ni kujihami zaidi kuliko kushambulia.
"Mbinu nyingi tunazotumia ni za kujihami. Mazoezini hatufundishwi
kucheza soka la kushambulia na badala yake kocha amekuwa akitumia muda mwingi
kutufundisha namna ya kukaba maadui katika maeneo yetu."alisema mchezaji
mmoja nyota katika nafasi ya kiungo.
"Mimi siyo msemeji, lakini sasa hivi inabidi niseme. Wachezaji
vilevile hatuko fiti. Tunafanya mazoezi kwa dakika chache, hatujawahi kucheza
mazoezi ya mechi miongoni mwetu. Uimara wa timu unaanzia mazoezini na sisi
hatuko imara." aliongeza staa huyo.
Nyota mwingine wa Simba anayecheza nafasi ya ushambuliaji alisema:
"Kutokuwapo Emmanuel Okwi na Patrick Mafisango (marehemu), siyo sababu ya
timu kufanya vibaya. Nadhani kocha (Liewig) abadili mbinu."
"Kuna mechi nyingi Okwi hakucheza na bado tulishinda. Mimi
sifurahishwi na jinsi tunavyocheza kwa kumtegemea mshambuliaji mmoja
mbele." alisema mshambuliaji huyo.
Nyota mwingine wa safu ya ulinzi alihoji mantiki ya viongozi na Benchi
la Ufundi kumsajili kipa wakati wa dirisha dogo, huku timu ikiwa na upungufu wa
wachezaji katika safu ya ushambuliaji.
Aidha, kiongozi wa msafara wa Simba na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji,
Zacharia Hans Pope amekuja na hoja tofauti na malalamiko ya wachezaji dhidi ya
kocha wao.
Hanspope amesema Simba imefungwa kwa sababu wapinzani wao Libolo
walijiandaa vizuri kwa mazingira yote, ndani na nje ya uwanja kulinganisha na
Simba.
"Yatasemwa mengi, lakini ukweli tumetolewa na timu yenye uwezo
kuliko sisi. Wenzetu wamefanya maandalizi mazuri. Kumbuka kuwa kwenye uwanja
wao wa nyumbani waliwahi kuichapa Orlando Pirates ya Afrika Kusini 3-0."
alisema Hans Pope.
No comments:
Post a Comment