Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka,
ametoa siku 30 kwa mmiliki wa jengo la ghorofa 16, lililopo Mtaa wa Indira
Gandhi katikati ya jiji, Ally Raza kulibomoa jengo hilo baada ya kubainika
alilijenga chini ya kiwango.
Kadhalika Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira imeiagiza Halmashauri
ya Manispaa ya Ilala, kufanya uchunguzi wa ubora wa majengo mengine matano
yanayomilikiwa na Raza ambaye pia ni mmiliki wa jengo lingine la ghoroga 16
lililoporomoka wiki iliyopita jijini Dar es Salaam kama yako katika viwango
vinavyokidhi.
Jengo hilo lililoporomoka lilisababisha vifo vya watu 36, majeruhi 17
na uharibifu wa mali ikiwamo magari linamilikiwa na Raza.
Jengo hilo lilikuwa likijengwa na Kampuni ya Lucky Construction Limited
ambayo ni mali ya Diwani wa Kata ya Goba (CCM) Wilaya ya Kinondoni, Ibrahim
Kisoki ambaye pia alijenga jengo jingine jirani na la awali, imetolewa amri ya
kufanyika kwa utafiti kubaini kama limekidhi viwango.
Profesa Tibaijuka akizungumza mbele ya Kamati hiyo walipofanya ziara
katika jengo hilo jana, alisema uchunguzi wa awali wa kuporomoka kwa jengo hilo
umebaini kuwa jengo lililoko mkabala, pia lilijengwa chini ya viwango.
“Ninaagiza jengo hilo kuwa libomolewe ndani ya siku 30 kwa gharama za
mmiliki na akikaidi atalipishwa faini ya asilimia mbili ya gharama ya
kuendeleza pasipokuwa na kibali kwa kila siku hadi atakapotekeleza agizo hilo,”
alisema Profesa Tibaijuka na kuongeza;
“Makazi haya yanatakiwa kujengwa majengo yasiyozidi ghorofa 10, lakini
katika hili ghorofa ambalo linatakiwa kubomolewa kwanza kiutaalamu
halikuzingatia vigezo kutokana na kujengwa kwenye kiwanja chenye mita 150
ambacho ni kidogo.”
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli alisema kuna taarifa
kwamba mmiliki wa jengo anamiliki majengo mengine ambayo hivi sasa yanakaliwa
na watu pia yamezua hofu, hivyo yanatakiwa kufanyiwa uchunguzi.
“Kutokana na majengo yake mawili ambayo tayari yameleta utata kwa
kuonekana kujengwa chini ya viwango, hivyo tunataka majengo mengine
anayomiliki, Manispaa ya Ilala iyafanyie uchunguzi mapema ili kuepusha madhara
ambayo yanaweza kutokea,” alisema Lembeli.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk Terezya
Huvisa amewataka watu wanaotaka kujenga majengo yenye zaidi ya ghorofa sita
kufika ofisini kwake kupata vibali vya ujenzi.
“Mtu yeyote anayetaka kujenga jengo zaidi ya ghorofa sita anatakiwa
kuomba kibali wizarani na wao kupitia Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC)
watatoa kibali cha kujengwa au kutojengwa kutokana na uchunguzi wa sehemu
husika,” alisema Dk Huvisa.
No comments:
Post a Comment