Baada ya Malawi kutangaza kujitoa katika mazungumzo ya mgogoro wa mpaka
kati yake na Tanzania kwenye Ziwa Nyasa, Serikali imeitaka nchi hiyo kuacha
kutapatapa na kamwe isithubutu kugusa eneo hilo la mpaka.
Imesema kama nchi hiyo itakiuka, Serikali ya Tanzania itaomba ushauri
wa nini cha kufanya kutoka kwa jopo la usuluhishi wa sakata hilo linaloundwa na
marais wa zamani barani Afrika, Festus Mogae (Botswana),Thabo Mbeki (Afrika
Kusini) na Joachim Chissano (Msumbiji) ambaye ndiye mwenyekiti.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe alisema, “Nadhani watasikia na kuelewa, Serikali ya
Malawi iache kutapatapa, nchi zote ilikoenda kulalamika kuhusu mgogoro huu,
Tanzania tumekuwa tukielezwa na hata hao wanaotueleza wanaishangaa sana
Malawi.”
Kauli hiyo ya Serikali imekuja siku chache baada ya Rais wa Malawi,
Joyce Banda kusema kuwa mgogoro huo sasa utapelekwa katika Mahakama ya
Kimataifa ya Haki (ICJ), kwa madai kwamba juhudi za usuluhishi wa kidiplomasia
zimeshindikana.
Hata hivyo, uamuzi huo wa Malawi ni kinyume na makubaliano baina ya
nchi hizo mbili yaliyofanyika Novemba 7 mwaka jana, jijini Dar es Salaam ambapo
zilikubaliana kwamba jopo hilo ndiyo sehemu ya mwisho ya makubaliano.
Katika maelezo yake, Rais Banda alisema nchi yake imejitoa katika
mazungumzo ya usuluhishi kwa madai ya kuhujumiwa na Katibu wa jopo hilo ambaye
ni Mtanzania, John Tesha kwa maelezo kuwa anavujisha taarifa muhimu za Malawi
kwa Tanzania kabla ya Tanzania haijawasilisha taarifa zake kwa jopo hilo.
Akitoa ufafanuzi wa kina juu ya mgogoro huo Membe alisema hilo
lilionekana na ndiyo maana ulitolewa uamuzi kwamba nafasi ya Tesha itachukuliwa
na Leonard Simao ambaye ni waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Msumbiji.
“Mwanzo walisema kuwa Tanzania tunataka kuwavamia, tukatoa ufafanuzi
kuhusu jambo hilo, baadaye wakaibuka tena na kusema kuwa tumetengeneza ramani
ili kubadili eneo la mpaka, pia tulitoa ufafanuzi kuwa ilikuwa mipaka ya nchi
na sasa wamekuja na jambo jingine. Novemba 17 mwaka jana tulikubaliana na hiki
wanachokifanya Malawi ni kinyume na makubaliano. Ninawaomba waheshimu
makubaliano yetu, hata kama jopo likitoa uamuzi wa kesi kupelekwa ICJ, Tanzania
hatutakwenda mpaka tukutane na Malawi. Sasa kwa nini wao wanatapatapa?” alihoji
Membe.
Alisema kuwa tangu kuibuka kwa mgogoro huo, Malawi imekwenda kulalamika
katika nchi za Uingereza, Marekani, Umoja wa Afrika (AU) na katika Jumuiya ya
Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Huku akizungumza kwa ukali Membe alisema; “Wakati tunasubiri jopo
lifanye kazi yake tunaiomba Malawi isiguse eneo la mpaka katika Ziwa Nyasa, na
iwe hivyo hadi jopo au ICJ itakapotoa uamuzi.”
Mgogoro ulivyoanza
Mgogoro huo uliibuka baada ya Serikali ya Malawi bila kushauriana na
Tanzania ilitoa leseni kwa kampuni mbili za kigeni kutafuta mafuta katika eneo
la ziwa ambalo linamilikiwa na Tanzania.
No comments:
Post a Comment