Language

Sunday 3 March 2013

HABARI MUHIMU: WASOMI NA WANAHARAKATI WAMEMGOMEA KIKWETE

SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwaagiza Polisi,wakuu wa mikoa na wilaya kutofanya ajizi kwenye suala la wachochezi wa kidini , badala yake wachukue hatua stahiki,baadhi ya wasomi na wanaharakati wamepinga kauli hiyo na kudai  ni maneno ya kisiasa.
Wamedai kuwa kuanzia Serikali ya Awamu ya Tatu hadi hii ya nne zimekuwepo kauli za kupiga marufuku kashfa dhidi ya dini nyingine lakini kukashifiana kumekuwa kukifanyika  tena  kwa uwazi bila hatua kuchukuliwa.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, walitoa mifano ya kuwepo na mihadhara, CD, DVD na vipeperushi vya uchochezi na kashfa dhidi ya dini lakini hakuna anayechukuliwa hatua.
Kwa kuwa mambo haya yamekuwa yakifanyika muda mrefu bila hatua kuchukuliwa wameshauri  Polisi,wakuu wa mikoa,wilaya na usalama wa taifa wachukuliwe hatua kwa kushindwa kusimamia sheria na sasa amani ya nchi inaingia shakani.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana amesema kauli aliyoitoa Rais Kikwete ni kauli ya kisiasa na alitakiwa  kutoa tamko la  kuwawajibisha watendaji wake pindi wanaposhindwa kutekeleza wajibu wao.
Alisema  vitendo hivi vyote vya machafuko ya kidini vinafanyika hadharani huku  wakuu wa mikoa,wilaya na  Usalama wa taifa wakishuhudia wakati jukumu la  kulinda amani katika eneo husika ni lao.
Naye  Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama Cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro anasema Serikali inayoongozwa na CCM haina uwezo wa kutokomeza udini.
Katika hotuba yake ya kawaida ya kila mwisho wa mwezi aliyoitoa Februari 28, mwaka huu, Rais Kikwete aliiagiza Polisi nchini kukamilishe mapema upelelezi wa makosa ya vurugu za kidini na wahusika wafikishwe haraka kwenye vyombo vya sheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Aliwataka wakuu wa mikoa nao kutoona ajizi katika hilo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...