Halmashauri Kuu ya Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini na bodi ya
wadhamini wa mali za kanisa hilo, wametoa tamko zito la kumtaka
Mwenyekiti wa Jimbo la Misheni Mashariki aliyesimamishwa, Mchungaji
Clement Fumbo kurudisha mali za kanisa na kuacha kujihusisha na shughuli
za kanisa hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jimbo la Kusini, Clement Mwaitebele alisema alichokifanya Mchungaji Fumbo ni ubatili mkubwa na kwamba ni kitendo kinachohatarisha amani ya Watanzania, hivyo kama viongozi wakuu wa kanisa wameamua kuingilia kati.
Alisema barua za kumtaka afanye hivyo tayari zimeshaandaliwa na kwamba akikaidi kurudisha ofisi, kuondoka katika Jengo la Usharika wa Tabata na
kurudisha mali nyingine za kanisa atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kumfungulia kesi mahakamani.
Sambamba na hilo, alisema wanatarajia kuwa na kikao leo na wachungaji wote wa eneo la Misheni, lengo likiwa ni kukubaliana nao jinsi ya kufanya kazi, atakayekiuka misingi iliyowekwa atatakiwa kuondoka katika majengo ya kanisa na kurudisha fedha alizosomeshewa na kanisa na akikaidi atawajibishwa kisheria.
Alisema awali mkutano mkuu wa kanisa Jimbo la Misheni ulioketi Oktoba 5-6 mwaka jana, ulitoa uamuzi wa kuondolewa madaraka kwa Mchungaji Fumbo na kuachishwa uchungaji, ambapo Oktoba 10 mwaka jana aliandikiwa barua ya kumtaarifu maazimio hayo.
Alisema kufuatia mkanganyiko huo, Umoja wa Kanisa Duniani (Unity Board), walitembelea Jimbo la Misheni lengo likiwa kujionea kama wapo tayari kupewa cheti cha kuwa jimbo kamili, lakini walikuta malumbano na kushauri kupatikana kwa suluhu kwa lengo la kuimarisha umoja katika kanisa .
Alisema jimbo la Kusini ni jimbo linaloongoza maeneo ya Tukuyu, Kyela, Ileje, Zanzibar, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro, Ruvuma, Iringa, Mtwara na Lindi, hivyo wameamua kuingilia kati suala hilo kwani kwa sasa linaelekea kuvuruga amani.
Alisema katika kujitanua zaidi na kuwa karibu na Wakristo, waliazimia kulitenga eneo la Mashariki yaani Dar es Salaam, Mtwara, Lindi, Pwani, Zanzibar na Morogoro ili lianze kutafuta uhalali wa kuwa jimbo kamili, kwani kwa sasa bado halina cheti cha utambulisho wa kuwa jimbo kamili na ndiyo maana linaitwa Jimbo la Misheni Mashariki.
Alisema kanuni na katiba ya kanisa hilo kifungu
cha 2 kinaeleza wazi kuwa jimbo la Misheni litachagua halmashauri kuu ya
kuliongoza, lakini litawajibika kwa jimbo mama ambalo ndilo jimbo la
Kusini hadi litakapokuwa jimbo kamili.
Mchungaji Mwaitebele alisema vurugu za uongozi na
madaraka zilipoanza kutikisa, waliamua kuingilia kati kama wasimamizi
halali wa eneo hili la Misheni,ambapo waliweza kukaa vikao vingi bila
kupata suluhu kwani mara nyingi Mchungaji Fumbo alipoitwa alikaidi.
Alisema kwa kuzingatia katiba ya kanisa kifungu
namba 11 kipengele cha C kinachoeleza wazi kuwa mkutano mkuu wa kanisa
(Sinodi), waweza kuitishwa wakati wowote na halmshauri kuu ya jimbo
kujadili jambo la dharura, lakini itatoa taarifa kwa wajumbe wake kwa
muda wa miezi miwili.
Alisema Sinodi imepewa mamlaka kikatiba kifungu
cha 10 kipengele cha M na N kutoa maamuzi ye mwisho ya kila Mkristo au
kila chombo chochote kilicho chini yake, hivyo alisema mambo yote
yaliyokuwa yakitekelezwa na viongozi yalikuwa sahihi kikatiba.
Aliongeza kuwa kifungu cha katiba namba 99
kipengele cha A - B kinafafanua kuwa makamu mwenyekiti atasimamia
shughuli zote za kanisa atakazopangiwa na mwenyekiti, pia atafanya
shughuli za mwenyekiti kama akiwa amesafiri ndani ama nje ya nchi.
Hivyo alisema maamuzi yote ikiwa ni pamoja na
kufanyika kwa sinodi ya dharura hayapo nje ya katiba kama inavyopotoshwa
na baadhi watu.
Ametoa wito kwa waumini wa kanisa kuwa watulivu
kipindi hiki, huku wakimuomba Mungu anayeweza kutuliza dhoruba aweze
kusimamia suluhu ndani ya kanisa hilo.
No comments:
Post a Comment