Wanasheria wa rais mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta, wameiomba Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Jinai, ICC, kumfutia mashitaka yanayomkabili mbele ya
mahakama hiyo.
Bwana Kenyatta amekanusha kuchochea ghasia baada ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2007.
Kikao maalum cha mahakama hiyo kimefanyika wiki moja baada ya mashitaka
dhidi ya mshtakiwa-mwenza, Francis Muthaura, kutupiliwa mbali na mahakama ya
ICC.
Mawakili wa Kenyatta wanasema kuachiwa kwa Muthaura, pia kunafuta
mashitaka dhidi ya Kenyatta, lakini mwendesha mashitaka wa ICC amesema ana
ushahidi zaidi dhidi ya Uhuru Kenyatta.
Kesi dhidi ya Bwana Kenyatta, ambaye alishinda uchaguzi mkuu
uliofanyika mapema mwezi huu, na kutangazwa rais mteule baada ya kupata
asilimia kidogo juu ya 50%, imepangwa kuanza kusikilizwa mwezi Julai.
Baada ya matokeo ya uchaguzi wa Desemba mwaka 2007 - wakati Bwana Raila
Odinga aliposhindwa dhidi ya Rais wa sasa Mwai Kibaki, zaidi ya watu 1,000
waliuawa na wengine 600,000 kuachwa bila makaazi.
Bwana Kenyatta, mtoto wa mwasisi wa taifa la Kenya, Jomo Kenyatta
anatuhumiwa kupanga mashambulio dhidi ya makundi ya kikabila yaliyokuwa
yakimuunga mkono Bwana Odinga kufuatia uchaguzi wa mwaka 2007.
No comments:
Post a Comment