Hatimae Marekani imethibitisha kuwa Muasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo, Jenerali Bosco Ntaganda, amejisalimisha katika ubalozi wake mjini
Kigali, Rwanda.
Taarifa hiyo ya Marekani inasema kuwa Ntaganda ameomba ahamishwe hadi
katika Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa ICC huko the Hague.
Ntaganda aliyeanzisha maasi nchini Congo ameshitakiwa katika mahakama
hiyo ya ICC na anakabiliwa na mashitaka ya kuwajumuisha watoto katika jeshi,
mauaji na ubakaji.
Jenerali Ntaganda mwenyewe anakanusha madai hayo yote.
Marekani imesema kwa wakati huu inashauriana na serikali kadhaa ili
kufanikisha ombo hilo la Jenerali Ntaganda ahamishwe hadi mahakama ya ICC.
Awali Serikali ya Rwanda ilikuwa imetangaza kuwa Jenerali huyo muasi
anayetuhumiwa kuhusika na uhalifu wa kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo amejisalimisha katika ubalozi wa Marekani mjini Kigali, Rwanda.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo amesema taarifa
walizonazo ni kuwa Kiongozi huyo muasi yuko chini ya ulinzi wa Marekani katika
ubalozi wake.
"Tumefahamishwa hii leo (Jumatatu) kuwa Bosco Ntaganda ameingia
Rwanda na kujisalimisha katika Ubalozi wa marekani hapa Kigali", amesema
Louise Mushikiwabo
Jenerali Ntaganda amekanusha mashitaka yanayomkabili katika mahakama ya
Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai ICC kwamba anahusika na uhalifu wa kivita na ule
dhidi ya binadamu.
No comments:
Post a Comment