Wawakilishi kutoka mataifa 150 wanakutana leo mjini New York Marekani,
katika shinikizo la mwisho la kuunda mkataba wa kimataifa, unoalenga kukomesha
uuzaji wa silaha kiholela, lakini Marekani inashinikizwa kuukataa.
Wanaharakati wa udhibiti wa silaha na watetezi wa haki za binaadamu
wanasema mtu mmoja anakufa kila dakika duniani kote kutokana na vurugu
zinazohusiana na silaha, na kwamba kunahitajika mkataba unaoyafunga mataifa
kudhibiti uuzaji wa silaha kiholela, ambazo wanasema huchochea vita, ukatili na
ukiukaji wa haki za binaadamu.
Biahsara ya silaha ina thamani ya dola za Marekani bilioni 70 kwa
mwaka.
Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa ulipiga kura mwezi Desemba kuanzisha
tena majadilano wiki hii, juu ya kile kinachoweza kuwa mkataba wa kwanza wa
kimataifa wa kudhibiti biashara ya silaha yenye thamani ya dola za Marekani
bilioni 70 - kuanzia meli za kivita, vifaru na helikopta za mashambulizi, hadi
kwenye bunduki za kawaida. Hii ni baada ya mkutano wa awali uliofanyika mwezi
Julai mwaka 2012, kuvunjika kwa sababu Marekani, na baadaye Urusi na China, zilitaka
zipewe muda zaidi.
NRA yamshinikiza Obama aukatae
Wajumbe wa mkutano wa Julai walisema utawala mjini Washington ulitaka
kusogeza suala hilo mbele ya uchaguzi wa rais uliyofanyika mwezi Novemba ingawa
serikali ya Obama ilikanusha madai hayo. Majadiliano ya sasa yatakwenda hadi
Machi 28. Marekani inasema inahitaji mkataba imara, lakini rais Obama yuko
chini ya shinikizo kutoka kwa chama chenye nguvu cha wamiliki wa silaha nchini
humo, NRA, kuzuia mkataba huo. Chama hicho kimeapa kuwa kitazuia kuridhiwa kwa
mkataba huo ndani ya baraza la Seneti, kama utawala wa Obama utauunga mkono
ndani ya Umoja wa Mataifa.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry, alionyesha yuko
tayari kuunga mkono mkataba huo kwa masharti siku ya Ijumaa, akisema Marekani
bado inasimamia dhamira yake ya kupatiakana kwa mkataba imara na wenye ufanisi,
utakaosaidia kushughulikia madhara makubwa ya biashara hii ya silaha kwa amani
na utulivu wa dunia. Lakini alirudia kuwa Marekani, ambayo ndiyo nchi ya kwanza
duniani kwa kutengeneza silaha, haitaukubali mkataba unaoingilia haki ya raia
wa Marekani kumiliki silaha, jambo ambalo ni nyeti sana kisiasa nchini humo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema serikali yake
itaunga mkono mkataba wa udhibiti wa silaha kwa masharti.
Lengo la mkataba
Lengo la mkataba huu ni kuweka viwango vya uhamishaji wa silaha zozote
zinazovuka mipaka, ziwe nzito au nyepesi. Mkataba huo utaweka pia masharti kwa
mataifa kuangalia upya mikataba ya silaha, kuhakikisha hazitumiki katika
ukiukaji wa haki za binaadamu, kukiuka vikwazo vya kimataifa na hazibadilishwi
matumizi kinyume na sheria.
Wanadiplomasia wanasema iwapo mkataba huo utashindwa kupata uungwaji
mkono unaohitajika kwa sababu Marekani, Urusi au nchi nyingine inayotengeneza
silaha kwa wingi inaupinga, mataifa yanaweza bado kuupigia kura ndani ya baraza
la Umoja wa Mataifa. Chaguo lingine ni kuurekebisha mswada huo na kuufanya
ukubalike na Marekani na wajumbe wengine.
No comments:
Post a Comment