Dereva wa gari lililomgonga na kumuua askari wa usalama barabarani,
Elikiza Nko atafikishwa kortini wakati wowote baada ya
upelelezi kukamilika, ilielezwa jana.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini(trafiki), Mohammed Mpinga
alisema hayo jana alipozungumzia tukio hilo ambalo lilisababisha simanzi kwa
watu wengi.
Mpinga alisema polisi walifanikiwa kumkamata mhusika kwa mbinu za
kipolisi na kwamba kwa jana alikuwa akihojiwa ili kupata ushahidi utakaowezesha
kumpeleka kortini.
Alisema dereva huyo ni kati ya wale wawili waliowakamata
awali na hatimaye mmoja walimbaini kuwa ni mhusika .
‘’Juzi usiku tuliwahoji na mmoja wao alitudanganya, tulipomuuliza
dereva wa gari hili ni nani akajibu siyo mimi nimeachiwa na mwenyewe amekimbia”
alisema Kamanda Mpinga na kuongeza kuwa baada ya kumbana alikiri kuwa ndiye.
Kwa mujibu wa Kamanda Mpinga marehemu ameacha mume na watoto watatu.
Maziko yanatarajiwa kufanyika leo katika makaburi ya Mbweni yaliyopo Manispaa
ya Kinondoni na yatahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa.
Marehemu alifariki dunia baada ya kugongwa na gari lililokurupuka
kuufuata msafara wa Rais Jakaya Kikwete eneo la Bamaga Mwenge jijini Dar es
Salaam Jumatatu iliyopita alipokuwa katika ziara ya kutembelea mkoa huo.
No comments:
Post a Comment