Mahakama ya juu kabisa nchini India leo imemhukumu mwigizaji filamu za
Kihindi maarufu kama Bollywood, Sanjay Dutt, kifungo cha miaka mitano gerezani
kwa kupatikana na silaha ambazo zilikuwa sehemu ya shehena ya silaha
zilizotumiwa katika shambulio la mjini Mumbai mwaka wa 1993.
Mahakama hiyo ilishikilia hukumu ya Dutt iliyotolewa na mahakama ya
kupambana na ugaidi mwaka wa 2007, lakini ikapunguza kifungo chake cha miaka
sita. Mahakama hiyo ya juu kabisa India pia imeshikilia hukumu ya kifo
iliyotolewa kwa Yakub Abdul Razzak Memon, kaka yake mshukiwa aliyepanga
mashambulio hayo, Tiger Memon, na kubadilisha hukumu za kifo dhidi ya watu kumi
kuwa kifungo cha maisha gerezani kufuatia shambulizi hilo. Maafisa wa ujasusi
wanasema Tiger Memon pamoja na mshukiwa mwingine Dawood Ibrahim, ndio
waliopanga shambulizi hilo, na bado wako mafichoni, wakiaminika kujificha
nchini Pakistan. Milipuko ya bomu iliyapiga maeneo 13 mjini Mumbai, ikiwa ni
pamoja na jengo kuu la soko la hisa, hoteli tatu na masoko kadhaa yenye
shughuli nyingi, mnamo Machi 12 mwaka wa 1993, na kuwauwa watu 257. Watu
wengine 800 walijeruhiwa.
No comments:
Post a Comment