Wakimbizi 74 elfu wa Mali wamekwama katika jangwa la Mauritania
wakikumbwa na ukosefu wa maji na idadi ya vifo vya watoto ikizidi
kuongezeka,linasema shirika la madaktari wasiokuwa na Mipaka-Medecins Sans
Frontiere.
Mzozo wa Mali umepelekea zaidi ya watu laki mbili na 70 elfu kuyapa
kisogo maskani yao na kuranda randa ndani nchini huku wengine zaidi ya laki
moja na 70 elfu wakikimbilia katika nchi jirani na hasa Burkinafasso,Mauritania
na Niger.
Katika jangwa la Mauritania ambako hali ya hewa inapindukia nyuzi joto
50 kivulini, kambi ya wakimbizi ya Mbera inawapokea watu 74 elfu
"walionasa jangwani" - kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Madaktari
Wasiokua na Mipaka-Medecins Sans Frontièren-MSF.Watu hao wamekimbia
mapigano,chuki za kikabila,ukosefu wa chakula na kuvurugika mfumo wa huduma za
jamii.
Ripoti hiyo inazungumzia kuhusu "hali mbaya kupita kiasi"
inayowakumba watu hao wanaotegemea moja kwa moja msaada kutoka nje kuweza
kunusurika. "Chakula kipo cha kutosha,lakini hakuna maji"- amesema
Marie-Christine Ferir anaesimamia operesheni za dharura katika shirika hilo la
madaktari wasiuwa na mipaka.
Watoto walioanza kuingia katika kambi hiyo tangu januari mwaka huu,hali
yao ya afya imeharibika na wanaonyesha dalili za ukosefu wa lishe bora-amesema
bibi Marie-Christine Ferir na kuongeza watoto kati ya 23 na 24 wanakufa kila
siku katika kambi ya Mbéra.
Mazungumzo ya kuleta suluhu yaharakishwe
Katika ripoti yake shirika la Medecins Sans Frontiere-MSF inasisitiza
juu ya umuhimu wa kuendelea kutolewa misaada kwa wakati wote unaohitajika.
"Mivutano ya kikabila na kisiasa ndiyo chanzo cha hali hii na
hakuna dalili kama wakimbizi watarejea nyumbani haraka" shirika la MSF
limesema.
Ili kumaliza mzozo,shirika la kimataifa linalosimamia mizozo
limeihimiza serikali ya mjini Bamako ianzishe haraka juhudi za kuzipatanisha
jamii nchini Mali.Miongoni mwa mengineyo shirika hilo linaisihi serikali ianze
mazungumzo na jamii ya watuareg na waarabu.
Uchaguzi utaitishwa Julai
Wakati huo huo waziri mkuu Diango Sissoko wa Mali akiwa ziarani Gao
amesema uchaguzi utaitishwa kama ilivyopangwa mwezi Julai mwaka huu licha ya
shaka shaka kama serikali itaweza kweli kudhibiti hali ya mambo katika maeneo
ya kaskazini ya nchi hiyo.
Hiyo ilikuwa ziara ya kwanza kuwahi kufanywa na kiongozi wa serikali
tangu vikosi vya Ufaransa vilipoanzisha opereshini ya kuwaandama wanamgambo wa
itikadi kali Januari mwaka huu.
No comments:
Post a Comment