Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM), jana aliwavunja mbavu
wabunge baada ya kuitaka Serikali kutoa tamko la kuruhusu bangi kuwa zao halali
la biashara kwa manufaa ya nchi na wananchi wake.
Keissy ambaye amezoeleka bungeni kama mzee wa kulipua mabomu, alitoa
kauli hiyo kupitia swali lake la nyongeza ambapo alisema zao la tumbaku nchini,
halina maana kwa sasa zaidi ya bangi.
“Mimi naona hakuna sababu ya kuendelea kusimamia mazao ambayo hata
dunia nzima wanayakataa kwa sababu yana ugonjwa wa kansa, leo Serikali itoe
tamko ni lini itaruhusu zao la bangi kulimwa kama zao la biashara ili wananchi
walime kwa uhuru,” aliuliza Keissy.
Alisema kuna faida kubwa katika kulima bangi kuliko kuendelea kulima
zao ambalo watu wengine duniani wameliona kuwa halifai.
Katika swali lake la msingi, Mbunge wa Mpanda Vijijini, Selemani Kakoso
(CCM), alitaka kujua ni lini zao la tumbaku litaingizwa kwenye ruzuku ya
Serikali ili kupunguza gharama za pembejeo kwa wakulima wa zao hilo.
Mbunge huyo pia alitaka kujua ahadi ya Serikali ya kupunguza ushuru
kutoka asilimia tano hadi kufikia asilimia mbili itatekelezwa lini.
Akijibu maswali hayo kwa pamoja, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Adam Malima alikiri kuwa zao la tumbaku ni zao ambalo linaingiza
fedha nyingi za kigeni kuliko mazao mengine ya biashara, lakini halina ruzuku
ya pembejeo kama ilivyo kwa mazao mengine.
Malima alisema kutopata ruzuku kwa zao hilo, kunatokana na ufinyu wa
bajeti na uwezo wa zao lenyewe kujihami.
Kuhusu bangi, alisema “Tanzania haijaweza kuhalalisha zao la bangi,
hivyo tusilinganishe na zao la tumbaku ambalo Tanzania limeonekana kuwa na
ubora wa kimasoko hadi China.”
No comments:
Post a Comment