Polisi mkoani Mbeya wanatuhumiwa kumshushia kipigo Barnabas Kahemele
akiwa mahabusu na kusababisha kifo chake.
Kufuatia tukio hilo, ndugu wa marehemu Kahemele wamegoma kuuchukua
mwili wa marehemu huyo uliohifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa
Mbeya wakidai kwamba mazingira yanaonyesha kuwa kifo chake kimetokana na kipigo
cha polisi baada ya kumkamata.
Inadaiwa kuwa marehemu na wenzake wawili walikamatwa usiku ya Jumatano
wiki hii, baada ya askari hao kufika nyumbani kwa marehemu, eneo la Uyole ya
Kati. Mke wa marehemu Sara Muhwanji, alidai kuwa wakiwa wamelala walisikia mtu
akigonga hodi na ndipo alipoamka na kutoka sebuleni.
“Nilitoka sebuleni na kuuliza nani anayegonga, ndipo nikasikia sauti ya
mtu anasema kuwa mimi Mhagama, huyo ni jirani yetu pale nyumbani. Lakini
sikufungua mlango na nikaenda kumwamsha
mume wangu, naye akauliza nani jibu
likawa mimi Mhagama nina shida, fungua mlango. Ndipo marehemu alipofungua
mlango, polisi wanne wakaingia ndani na kumwambia kuwa yupo chini ya ulinzi,”
alisema Sara.
Alifafanua kuwa baada ya hapo polisi hao waliondokana naye na kwamba
alipojaribu kuhoji kosa alijibiwa kuwa afike polisi asubuhi ataambiwa kosa la
mume wake. “Nilipofika asubuhi ambayo ni juzi Alhamisi nikauliza mapokezi na
kuwaambia kuwa nimekuja kumwona mume wangu, askari wa mapokezi wakatafuta jina
lake lakini hawakuliona,” alisema.
Alieleza kuwa baada ya hapo askari walimfuata na kumchukua, kisha
kumpeleka ofisi zilizo ghorofani na wakamwingiza kwenye chumba cha mahojiano,
ambapo alihojiwa na askari wa kiume.
Alisimulia kwamba baada ya kumaliza walimtaka aendelee kukaa kituoni
hapo akisubiri taratibu zinazoendelea kuhusu mume wake.
Alisema kuwa baada ya muda mfupi majibu yakawa tofauti na kuambiwa kuwa
imetokea bahati mbaya mume wake amefariki dunia.Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mbeya, Barakael Masaki alipohojiwa kwa njia ya simu kuhusu tukio hilo alisema
kuwa hana taarifa.
No comments:
Post a Comment