VIWANDA vinne vya kutengeneza pombe, kusindika maziwa na machinjio mawili
yamefungwa katika wilaya za Rombo, Mwanga na Siha mkoani Kilimanjaro kutokana
na kushindwa kukidhi vigezo vya ubora vilivyoainishwa na Mamlaka ya Chakula na
Dawa nchini (TFDA).
Mkaguzi wa Chakula Kanda ya Kaskazini, Abdalah Mkanza alisema
ufungaji huo umefanikiwa wakati idara ya ukaguzi ya kanda hiyo ilipofanya
ukaguzi wa kushitukiza kwa kushirikiana na wakaguzi wengine kutoka Kanda ya
Mashariki.
Alisema ukaguzi ulifanyika kwa viwanda vyote vikubwa na vidogo mkoani
Kilimanjaro na machinjio yote za mjini na vijijini ambapo walibaini wananchi
wapo hatarini kupata magonjwa kutokana na mazingira halisi ya uchinjajio wa
wanyama na viwanda hivyo.
Mkaguzi huyo alisema zoezi la ukaguzi litafanyika kwa mara nyingine
mkoani humo kwa lengo la kutazama iwapo maeneo waliyoyapa maelekezo yamefuata
ama la, ili hatua nyingine ziweze kuchukuliwa iwapo itabainika wamepuuza.
Aliwataka wafanyabiashara na waagizaji wengine wa bidhaa kutoka nje ya
nchi kuwasiliana na TFDA ili kujiridhisha kama wanavyoagiza au kutumia kwa
ajili ya walaji vimethibitishwa na mamlaka hiyo.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliohojiwa kuhusiana na kufungwa kwa
viwanda vya pombe, Johnson Swai na Habibu Juma walipongeza juhudi hizo lakini
wakataka ukaguzi huo kufanyika kila baada ya miezi sita kwani wapo wanaofungua
viwanda na kufunga mara wanaposikia wakaguzi wanapita.
No comments:
Post a Comment