Language

Friday 11 January 2013

HABARI: MCHUNGAJI MTIKILA AFUFUA MAPYA KATIKA MCHAKATO WA KUTOA MAONI YA KATIBA MPYA


MAKUNDI maalumu jana yaliendelea kutoa maoni yao kwenye mchakato wa Katiba Mpya, huku DP kikipendekeza Rais aapishwe baada ya siku 90 tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu.
 Mbali na maoni hayo yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Mchungaji Christopher Mtikila, makundi mengine; wakulima, wafugaji, wanahabari na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) nayo yalijitokeza kutoa moyoni.Mtikila alisema kipindi hicho cha siku 90 kitatoa fursa kwa watu wanaotaka kuwasilishapingamizi dhidi ya ushindi wa Rais mteule kufanya hivyo, kabla ya kuapishwa.Alisema pingamizi linaweza kufanyiwa kazi kwa kipindi hicho cha miezi mitatu ili kuhakikisha kuwa taifa linapata kiongozi halali mwenye ridhaa ya wananchi.
“Pia tunataka kinga ya Rais ikome pale anapomaliza muda wake wa uongozi, kama alifanya makosa yoyote ya jinai aweze kushtakiwa ili kujenga nidhamu ya uongozi katika ofisi ya umma. Utaratibu wa kumwondoa madarakani uimarishwe asisubiriwe hadi amalize muda wake wa uongozi.”
Alisema kuwa Katiba ya nchi inapaswa kuwa mali ya wananchi wenyewe ili watawala wasijihusishe katika kuwaundia wananchi Katiba kama ilivyo kwa mchakato unaoendelea sasa wa kupata Katiba Mpya.
“Kumekuwa na hoja ya kuwapo kwa Serikali ya Tanganyika, hilo ni jambo muhimu na watu kutoka Tanganyika ni lazima wawe na Serikali yao ndani ya mipaka ya ardhi yao kupitia Katiba Mpya,” alisisitiza Mchungaji Mtikila.
Aliongeza kuwa nafasi za wabunge wa viti maalumu bungeni ziondolewe ili viti hivyo vishindaniwe kidemokrasia. Alisema wanawake wanatakiwa waelimishwe na kupikwa ili wahimili ushindani katika medani za kisiasa. Alisema kuwa taifa linahitaji viongozi bora na siyo kustarehesha jinsia.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...