Language

Wednesday 6 February 2013

BURUDANI: NI KWELI ADAM KUAMBIANA ANA TABIA KAMA ZA BALOTELI? SOMA BARUA HII



Adam Kuambiana.
KWENU,
Watayarishaji na wasanii wa filamu Bongo. Naamini mnaendelea vyema na majukumu yenu ya kila siku. Mimi ni mzima wa afya. Nimekuja kwenu kwa lengo moja kubwa; kumzungumzia msanii mwenzenu Adam Kuambiana.

Nakumbuka kuna wakati niliwahi
kumwandikia barua tatu mfululizo, ni kwa sababu alifanya jambo ambalo halikubaliki na nikaamua kutumia kalamu yangu kumrudisha kwenye mstari. Siku zote huwa napenda kuegemea kwenye ukweli.
Werevu huuchukua ukweli wangu na kuufanyia kazi, wapumbavu hujenga chuki na pengine kupanga mambo mabaya dhidi yangu!  Hawatashinda maana vita hii si yangu peke yangu. Aliyeniumba yu pamoja nami katika kufanikisha kile chenye msingi wa haki.
Turudi kwa Kuambiana. Huyu jamaa nilimfahamu kwa mara ya kwanza wakati alipokuwa akirekodi Sinema ya Fake Pastors. Alicheza na Ray (Vincent Kigosi), Johari (Blandina Chagula), Jokate Mwegelo, Lisa Jensen na wasanii wengine wengi wenye majina makubwa.
Kama kumbukumbu zangu zitakuwa sawa, ilikuwa ni mwaka 2007. Nilipofahamiana naye kwa mara ya kwanza (ingawa kwa kidogo), niligundua jamaa ni muongeaji sana na anayependa kujisifia.
Filamu ile ilipotoka, alitisha. Alifanya kitu kikubwa sana. Baada ya hapo, akaanza kucheza filamu nyingine nyingi. Kwa kawaida huwa hafanyi makosa. Anajua anachokifanya anapokuwa nyuma ya kamera, sema sasa dah! Mkorofi sana. Balotelli wa Bongo!
Ni vigumu kukaa naye kwa muda mrefu bila kutofautiana. Ana maneno makali, hasira za haraka, hataki kurekebishwa, anajiamini kupita kiasi na pengine anadhani hakuna mwingine anayeweza kuwa kama yeye. Huyu ndiye Adam Kuambiana.
Ana msururu wa matukio ya ugomvi anapokuwa ‘location’. Makabrasha yangu yanaonesha amewahi kugombana na wenzake mara nyingi sana wanapokuwa eneo la kazi. Ipo listi ndefu ya aliotofautiana nao akiwa kazini.
Sina lengo la kuitaja hapa, lakini naamini wengi mnajua ninachozungumza. Hata yeye mwenyewe pia anafahamu. Ukiachana na wasanii wenzake, hata anapopigiwa simu na waandishi kwa ajili ya mzani wa habari, hataki. Atatoa maneno makali na ya kuudhi.     Nilipata kuzungumza naye na kwa kweli alionekana kuelewa, leo hii ni rafiki mzuri tu.
Pamoja na yote hayo mabaya niliyoyasema, huyu jamaa ana kitu kikubwa sana kichwani mwake. Ndiyo maana nikaamua kuwaandikia hii barua ili muweze kumtambua na kujua namna ya kufanya naye kazi. Je, ‘vurugu’ zake na kugombana ‘location’ zinatakiwa kuangaliwa kama kigezo cha kufanya naye kazi?
Je, asishirikishwe kwenye filamu yoyote kwa sababu nilizotaja hapo juu? Siyo kweli, kipo cha kufanya. Hicho ndicho nitakachowaeleza wiki ijayo kwa sababu leo nimeishiwa na makaratasi. Ahsante sana kwa kunisoma.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...