Language

Saturday 9 February 2013

HABARI MUHIMU: UFISADI WA SERIKALI WAANIKWA BUNGENI

BUNGE limebaini kuwapo kwa udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, huku likibainisha upotevu wa matrilioni ya shilingi, unaotokana na kutosimamiwa kwa sheria za kodi, misamaha ya kodi na udhaifu wa usimamizi wa sheria nyingine katika maeneo yenye rasilimali za taifa.

Ripoti ya Kamati Maalumu ya Spika, kuhusu vyanzo vya mapato ya
Serikali pamoja na matumizi yake iliyowasilishwa kwake jana inabainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2012/13 pekee, Serikali imepoteza kiasi cha Sh3.95 trilioni kutokana na kasoro katika ukusanyaji wa fedha za mapato.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew Chenge alisema kuna dosari nyingi katika mfumo wa Serikali wa ukusanyaji wa mapato, ambazo ikiwa zitapatiwa ufumbuzi fedha zinazotokana na vyanzo vya ndani zitaongezeka na kuondoa kabisa nakisi katika bajeti zake.
Kamati hiyo ya wajumbe 12 imetoa mapendekezo 24, ambayo kwa mujibu wa Chenge, ikiwa yatatekelezwa yataiwezesha Serikali kupata mapato ya ziada yanayofikia Sh14.86 trilioni katika bajeti zake za 2014/15 na 2015/16.
Chenge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge, alisema kwamba ununuzi wa magari makubwa na ya anasa usiozingatia gharama za uendeshaji wake dhidi ya hali ya kiuchumi ni miongoni mwa kasoro ambazo zinapaswa kuchukuliwa hatua.
“Kwa mfano, kwa miaka mitatu mfululizo, gharama za mafunzo, ununuzi wa mafuta na matengenezo ya magari zilikuwa kama ifuatavyo; Mwaka 2008/09 Sh685 bilioni, 2009/10 Sh530 bilioni na 2010/11 Sh537 bilioni,”alisema Chenge na kuongeza:
“Kwa mwaka wa fedha 2010/11 gharama hizi zilikuwa ni sawa na asilimia 4.6 ya bajeti yote. Hii ina maana kwamba, katika kipindi cha miaka mitatu (2008 - 2011) jumla ya Sh1.8 trilioni zilitumika kuhudumia magari ya Serikali pekee,… kiasi hiki hakijumuishi gharama za ununuzi wa magari hayo.”

Vyanzo vya mapato

Chenge alisema kwamba katika utafiti wao, walibaini kuwa mwenendo wa Serikali katika kuwekeza na kuviendeleza vyanzo mbalimbali vya mapato yake ni wa kusuasua na hauridhishi.
Alivitaja baadhi ya vyanzo hivyo kuwa ni umeme, bandari, viwanja vya ndege, reli, uvuvi, viwanda, misitu na utalii pia sekta ndogo za simu za mkononi, majengo, biashara za kimataifa na bidhaa za viwandani.
Upo ushahidi kuwa Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania inaongoza kwa kukusanya kiasi kidogo cha mapato ikilinganishwa na pato lake la taifa. Katika Afrika ya Mashariki pia, Tanzania inaongoza kwa kutumia kiasi kikubwa cha gharama za ukusanyaji wa mapato zikiwianishwa na pato la taifa,”alisema Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (CCM).
Aliongeza kwamba Tanzania ina kiasi kikubwa cha sekta isiyo rasmi iliyoachwa nje ya wigo wa kodi, hivyo kuathiri ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuongeza utegemezi katika misaada ya wahisani kwenye bajeti ya kila mwaka.
“Katika Afrika ya Mashariki Tanzania inaongoza katika kupata kiasi kidogo cha kodi ya mapato (corporate tax) kutoka kwa makampuni ya simu za mkononi,
”alisema Chenge.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...