Language

Sunday 24 March 2013

HABARI MUHIMU: CHADEMA HAKUNA MAANDAMANO TENA


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekubali kusitisha maandamano yaliyokuwa yafanyike leo kushinikiza kujiuzulu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne ya 2012.
Makubaliano yalifikiwa baada ya kikao cha Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Said Mwema na viongozi wa Chadema walioongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe kilichofanyika makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho, IGP Mwema alikuwa na Kamishna wa Operesheni wa Polisi, Paul Chagonja, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleimani Kova na maofisa wengine wa ngazi za juu wa jeshi hilo.
Mbowe katika ujumbe wa Chadema aliambatana na Katibu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Deogratius Munishi na Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene.
Taarifa ya pamoja ya polisi na Chadema iliyosainiwa na Makene na Msemaji wa Mkuu wa Polisi, Advera Senso ilisema baada ya kushauriana, walikubaliana kusitisha maandamano hayo ili kutoa nafasi ya wananchi kushiriki katika mapokezi ya ugeni wa Rais wa Jamhuri wa Watu wa China, Xi Jinping.
“Pia katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Chadema na IGP Mwema walikubaliana kufanya kikao cha pamoja ndani ya siku 14 ili kuona utaratibu mzuri utakaoweka namna nzuri ya kuwasiliana na kushirikiana pasipo migogoro kwa pande zote mbili, huku kila upande ukitimiza wajibu wake kwa masilahi ya taifa, “ ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Chadema waliingia katika mvutano mkali na polisi kutokana na kuzuiwa kwa maandamano yao, ambapo kabla ya makubaliano ya jana walikuwa wamesisitiza kwamba yangefanyika hata kama polisi wangetumia nguvu kuyazuia.     

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...